Mwanaume mmoja raia wa Ethiopia anaelezea jinsi alivyoteswa na wasafirishaji haramu wa binadamu alipokuwa akimtafuta mpwa wake katika njia ambayo sasa imepata umaarufu kutokana na hatari zilizooigubika —kutoka Pembe ya Afrika kupitia Yemen hadi Saudi Arabia.
Jamal, mwenye umri wa miaka takribani 30, alipoanza safari katika njia inayojulikana kama njia ya mashariki, hakuwa akifuatilia kazi, utajiri, au hadhi. La hasha! Alikuwa akimtafuta mpwa wake wa mwenye umri wa miaka 16, aliyepotea alipokuwa akijaribu kufika Saudi Arabia kupitia mojawapo ya njia hatari zaidi za uhamiaji duniani.
Chanzo cha watu kukimbia makwao licha ya hatari njiani
Kila mwaka, makumi ya maelfu ya Waethiopia husafiri kupitia njia hii, wakivuka maeneo kame ya Ethiopia na Djibouti, Ghuba ya Aden, na Yemen iliyokumbwa na vita.
Wengi hukimbia migogoro, ukosefu wa makazi, umaskini au madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Wengine huvutiwa na ahadi za uongo zinazosambazwa na wasafirishaji haramu wanaonufaika na hali ya kukata tamaa.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), njia ya mashariki imezidi kuwa ya kikatili, ikitawaliwa na utekaji nyara, unyanyasaji wa kifedha, na ukatili wa kimfumo.
Jamal akiwa kwenye makazi ya wahamiaji nchini Djibouti
Mpwa wa Jamal alikuwa miongoni mwa waliotekwa. Akiwa Yemen, watekaji wake walidai fidia au kikombozi. Familia ililipa, lakini mvulana huyo hakuwahi kuachiliwa.
Hivyo Jamal alienda kumtafuta.
“Sikuwa na chaguo,” anasema. “Ndugu yangu hakuwa na watoto wengine. Ilibidi nimfuate.”
Kutafuta walanguzi wa binadamu
Akiwa Yemen, Jamal alijiweka kwa makusudi katika njia ya wasafirishaji haramu, akitumaini wangempeleka mahali ambapo mpwa wake alikuwa anazuiliwa.
Mpango huo ulifaulu. Alikutana tena na mvulana huyo, ingawa alijifanya hamtambui ili kuepuka tuhuma. Jamal alipoanza kupanga kutoroka kutoka kwa watu hao, aliwasaidia pia mateka wengine kutoroka. Hata hivyo, kabla hajafanikiwa kujiokoa, alikamatwa.
Adhabu ilikuwa ya haraka na ya kikatili
Jamal alilazimishwa kushuhudia mateka wengine wakipigwa, kukatwa viungo, na kuchomwa moto.
Jamal akipatiwa matibabu ya majeraha yake kwenye makazi ya wahamiaji nchini Djibouti.
Kisha ikafika zamu yake. Watekaji wake walifunga miguu yake kwa plastiki na kuiwasha moto mara kwa mara. Majeraha hayo yalisababisha ulemavu wa kudumu, yakimuathiri vibaya jinsi anavyotembea, anavyolala, na jinsi anavyoishi na kumbukumbu za usiku huo.
Mapigano yawa upenyo wa kutoroka
Walifanikiwa kutoroka tu baada ya mapigano kuzuka kati ya makundi hasimu ya wasafirishaji haramu. Katikati ya vurugu hizo, Jamal na mpwa wake walikimbia.
Nguo zinazodhaniwa kutelekezwa na wahamiaji zimetapakaa katika jangwa la Djibouti.
Baada ya miezi kadhaa nchini Yemen, wakiweza kujikimu kwa kuosha magari ili kupata fedha za kuondoka, hatimaye Jamal alifika Djibouti. Huko alipelekwa katika Kituo cha Mwitikio kwa Wahamiaji cha IOM kilichoko Obock, ambapo alipata matibabu ya majeraha yake na msaada wa kisaikolojia ili kuanza kukabiliana na aliyoyapitia.
Kwa mara ya kwanza tangu mateso hayo, anasema, mtu aliuliza si tu alikotoka, bali pia jinsi alivyokuwa akikabiliana na hali hiyo.
Sasa Jamal anajiandaa kurejea Ethiopia.
Bado hajamwambia mama yake kilichotokea. Hata sasa, anajali zaidi kuhusu mama yake kuliko yeye mwenyewe.
“Aliniona nikiondoka nikiwa na afya njema,” anasema. “Nina wasiwasi atakaponiona hivi. Itabidi nimweleze kwa upole.”