
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kila Ndege ni Muhimu,Ufuatiliaji Wako Una Umuhimu”, ikisisitiza nafasi ya watafiti, jamii za wenyeji, wanafunzi, wapenda ndege na wananchi wa kawaida katika kukusanya taarifa zinazosaidia kuelewa hali ya ndege wanaohama duniani.
Katika ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya aina za Wanyamapori na Mimea Iliyo Hatarini Kutoweka CITES, Ivonne Higuero amesema ndege wanaohama ni viumbe wa kipekee wanaounganisha mifumo ya ikolojia, tamaduni na uchumi katika maeneo mbalimbali duniani kupitia safari zao ndefu za kuvuka mipaka ya nchi.
“Kuanzia bata aina ya Baikal teal hadi mwewe aina ya Broad-winged hawk, changamoto zinazowakabili ndege hawa zinahitaji ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha wanaendelea kuishi na kufanya safari zao za asili.”
Ameeleza kuwa taarifa zinazokusanywa kupitia uchunguzi wa wataalamu na wananchi wa kawaida zimekuwa msaada mkubwa katika kuandaa mikakati ya uhifadhi wa ndege wanaohama na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ikiwemo ule wa CITES.
Kwa mujibu wa Higuero, taarifa za kisayansi kuhusu ndege walioko kwenye orodha ya CITES ni muhimu ili kuhakikisha biashara ya kimataifa ya aina mbalimbali za ndege hao inafanyika kwa njia endelevu bila kuhatarisha uwepo wao.
“Ufuatiliaji unaofanywa na watu duniani kote unasaidia kutoa picha halisi ya namna ndege hawa wanavyoathiriwa na mabadiliko ya haraka ya dunia yetu. Kila taarifa ina umuhimu mkubwa katika juhudi za kuhakikisha ndege hawa wanaendelea kufanya safari zao kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Ameongeza kuwa ndege wengi wanaohama walioko kwenye orodha ya CITES wana thamani kubwa kiutamaduni, kimazingira na hata kijadi katika jamii mbalimbali, hivyo uhifadhi wao unahitaji maamuzi yanayotegemea sayansi na ushirikiano wa kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka huu pia yanaungwa mkono na malengo ya kimataifa ya kuhifadhi bayoanuai na maendeleo endelevu.