
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Brigedia Jenerali Esmaeil Qaani, amesema kuwa utawala wa Israel unapaswa kuanza kuzoea “mfumo mpya wa nguvu katika kanda,” akisisitiza kwamba hatua zilizoratibiwa na washirika wa Iran katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) zimepunguza kwa kiasi kikubwa matarajio ya usalama ya Israel.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya X s, Jenerali Qaani ametoa tathmini yake kuhusu matukio ya hivi karibuni ya kikanda kufuatia kile alichokitaja kuwa vita vya uchokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran. Alieleza kuwa kiwango cha uratibu kati ya makundi ya “Mhimili wa Muqawama” kinaongezeka, huku malengo kadhaa ya kimkakati ya Israel yakishindwa kufikiwa.
“Netanyahu alikuwa na ndoto ya kupanua kile alichokiita ukanda wa usalama katika eneo lote la kanda. Hata hivyo, moto wa busara na ujasiri kutoka kwa ndugu zetu wa Hezbollah upande wa kaskazini na Ansarullah upande wa kusini umefichua wazi ahadi za uongo ambazo utawala huo uliwapa walowezi wake,” alisema kamanda huyo wa IRGC.
Jenerali Qaani aliongeza kuwa maono ya makamanda wa muqawama waliouawa katika mapambano sasa yanaonekana kutimia.
Amesema: “Dhamira ya makamanda mashahidi wa muqawama imetimia: chumba cha operesheni cha muungano wa muqawama sasa ni kimoja.”
Akihitimisha ujumbe wake, Jenerali Qaani amewataka watawala wa Israel kukubali mabadiliko hayo ya kimkakati. “Ni vyema wakaanza kuzoea mfumo mpya wa kikanda.”
Punde baada ya Jenerali Qaani kutuma ujumbe huo, mtandao wa X umefunga akaunti yake ikiwa ni jaribio la kuzima sauti ya haki.
Marekani pamoja na utawala haramu wa Israel zilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran kwa kumuua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Imam Khamenei, pamoja na maafisa kadhaa waandamizi wa kijeshi na raia, tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mashambulizi hayo yalijumuisha mapigo makubwa ya anga yaliyolenga maeneo ya kijeshi na pia miundombinu ya kiraia kote Iran, na kusababisha vifo vya raia wengi, wakiwemo watoto wa shule pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Kwa kujibu, Jeshi la Iran lilianzisha operesheni za kulipiza kisasi, likilenga ngome za kijeshi, kijasusi na kiuchumi za Marekani na Israel katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa na pia katika kambi za kijeshi za Marekani katika ardhi za baadhi ya nchi za eneo, kwa kutumia mawimbi ya makombora na ndege zisizo na rubani.