Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesifu na kupongeza ujasiri wa taifa la Iraq wa kusimama bega kwa bega na watu wa Iran katika kipindi hiki cha uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Masoud Pezeshkian ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X leo Jumanne, akisema: “Waislamu wa Iraq wamesimama kishujaa bega kwa bega na Iran katika vita hivi visivyo vya haki; kusimama huku kidete hakutokani na ukuruba wa kijiografia, bali ni kwa sababu ya historia, utambulisho na maadili ya pamoja ya kidini.”

Ameendelea: “Ninawapa mkono wa heko wananchi, maafisa wa Serikali na wapiganaji wa Iraq huko Mesopotamia. Ninathamini uthabiti wenu na ninaheshimu kujitolea kwetu,” amesema Rais Pezeshkian. 

Wakati huo huo Rais wa Iran amesisitiza udharura wa kuendelea kusimama imara taifa na Serikali  dhidi ya wavamizi.

Rais Masoud Pezeshkian amesema pambizoni mwa kikao cha baraza la mawaziri kwamba ana matumaini na mustakbali wa nchi na kusisitiza umuhimu wa kundelezwa mapambano na wananchi na Serikali dhidi ya wavamizi.

Amesema: “Kwa pamoja, na kwa kutegemea nguvu na mshikamano wetu, tutasimama dhidi ya uvamizi wa kikatili wa maadui ili kukamilisha kwa heshima njia hii ya kihistoria na muhimu.”

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa wakati umefika wa kuwafukuza wanajeshi wa Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia. Sayyid Abbas Araqchi  amesisitiza kuwa adui mchokozi haheshimu wala kuwajali Waarabu au Wairani.

Abbas Araqchi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwamba: Iran inaiheshimu Saudi Arabia na kuitambua kama nchi ndugu.

“Operesheni zetu zinamlenga adui mchokozo ambaye hawaheshimu Waarabu wala Wairani, wala hana uwezo wa kudhamini usalama wa kanda hii. Hebu oneni tulichofanya kwa kamandi yao ya ulinzi wa anga,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *