Programu ya Samia Ubora Kliniki ni mpango maalum wa Serikali ulioanzishwa ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mpango huu unaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara na kutekelezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kuzalisha bidhaa bora na salama zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku ukilinda usalama wa wananchi.
Akizungumza kuhusu kuanzishwa na utekelezaji wa programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Ashura Katunzi, anasema mpango huo umeleta mabadiliko makubwa kwa wajasiriamali na kwa soko la bidhaa nchini.
“Samia Ubora Kliniki ilianzishwa ili kusogeza huduma za viwango na ubora karibu na wajasiriamali. Lengo letu ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa salama, bora na zenye ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kupitia mpango huu, tunawalinda walaji na wakati huo huo tunawajengea uwezo wajasiriamali kukuza biashara zao kwa kuzingatia viwango vya ubora,” anasema Dkt Katunzi.
Kupitia Samia Ubora Kliniki, TBS imetoa mafunzo bure kwa wajasiriamali 1,059 katika mikoa 15 nchini. Mafunzo hayo yalihusu uzalishaji wa bidhaa bora, ufungashaji sahihi, uongezaji thamani wa bidhaa pamoja na masuala ya masoko. Idadi kubwaya walionufaika ni vijana, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali katika kuwawezesha kiuchumi.
Dk Katunzi anafafanua kuwa, ili kulinda usalama wa walaji, TBS ilipima sampuli 800 za bidhaa za wajasiriamali bila malipo katika maabara zake. Bidhaa zilizokidhi viwango zilipewa Alama ya Ubora ya TBS, hatua iliyowawezesha wananchi kuzitambua kwa urahisi na kuzitumia kwa uhakika.
Aidha, bidhaa 192 zilitunukiwa vyeti vya ubora bila wajasiriamali kulipia gharama za ukaguzi na upimaji, na hivyo kufungua milango ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Dkt Katunzi anaendelea kusema kuwa katika kusogeza huduma karibu na wananchi, TBS imeanza ujenzi wa majengo ya maabara na ofisi za kanda katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Arusha. Ujenzi wa jengo la Dodoma umefikia zaidi ya asilimia 90, huku jengo la Mwanza likiwa asilimia 70. Kukamilika kwa majengo hayo kutapunguza muda na gharama za kupata huduma za upimaji na uthibitishaji wa ubora.
Meneja wa Kanda ya Kati wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Hamis Sudi akizungumza na wananchi wa Itigi mkoani Singida wakati wa utoaji elimu kwa wafanyabiashara wa vyakula na vipodozi.
“Hatua hii ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli kwa wakati,” anasema Dkt Katunzi.
Kwa upande wa matumizi bora ya nishati, TBS imeanzisha maabara maalum ya kupima ufanisi wa matumizi ya umeme kwa vifaa kama majokofu, viyoyozi, taa, runinga na feni. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za umeme kwa wananchi na kulinda mazingira.
Pia, Shirika limeendesha warsha 18 kwa wajasiriamali katika sekta za chakula, ujenzi, nishati safi, madini na vifungashio ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora.
Dkt Katunzi anaelezea, Utekelezaji wa Samia Ubora Kliniki unafanyika kwa ushirikiano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambazo ni SIDO, BRELA, TANTRADE, TIRDO na Tume ya Ushindani (FCC), hatua iliyowezesha wajasiriamali kupata huduma mbalimbali kwa pamoja kupitia mfumo mmoja.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Charles Thomas, mjasiriamali wa usindikaji wa unga lishe kutoka Dar es salaam, anaeleza namna Samia Ubora Kliniki ilivyobadilisha biashara yake.
“Kabla ya Samia Ubora Kliniki, sikuwa na uelewa wa viwango wala ufungashaji sahihi. Nilikuwa nauza bidhaa zangu kwenye soko la kawaida tu, ila baada ya kupata mafunzo na cheti cha ubora bure kutoka TBS, bidhaa zangu sasa zinauzwa kwenye maduka makubwa na mapato yangu yameongezeka,” anabainisha.
Mafanikio ya Samia Ubora Kliniki ndani ya siku 100 yanaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi wa viwanda unaozingatia ubora wa bidhaa na usalama wa walaji. Kupitia mpango huu, wajasiriamali wamepata ujuzi, masoko na vyeti vya ubora, huku wananchi wakinufaika kwa kupata bidhaa salama na bora.
Programu hii inaunga mkono utekelezaji wa Sera ya Viwanda, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa lengo la kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa na kuboresha maisha ya wananchi.