
Ifikapo saa 8:00 usiku, kesho Jumatano, Aprili Mosi, 2026, idadi ya timu 48 zitakazoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Marekani, Canada na Mexico zitakuwa zimekamilika rasmi.
Muda wa saa tano (5) tu, kuanzia leo saa 3:45 usiku hadi kesho saa 8:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki, mechi sita za mchujo zitakazochezwa katika miji tofauti duniani, utatoa washindi sita ambao wataungana na wengine 42 ambao tayari wameshajihakikishia tiketi ya kucheza mashindano hayo.
Mechi hizo sita zinaonekana zitakuwa za presha kubwa kwa vile timu zitakazoshinda zitajihakikishia tiketi na zile zitakazopoteza zitalazimika kusubiri tena hadi fainali za 2030.
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu ni baina ya Sweden itakayocheza na Poland kusaka tiketi moja ya Kombe la Dunia kupitia barani Ulaya.
Kupoteza kwa Poland kutamaanisha mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski hatocheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu na kinyume chake, maana yake nyota wa Sweden, Viktor Gyokeres, Alexander Isak na Anthony Elanga hawatocheza Kombe la Dunia 2026.
Bosnia & Herzegovina itacheza na Italia, Jamhuri ya Czech itakabiliana na Denmark na Kosovo itacheza na Uturuki.
Uhondo mwingine utakuwa nchini Mexico ambako timu nne za mabara tofauti zitawania tiketi mbili za Kombe la Dunia mwaka huu.
Kuanzia kesho saa 6:00 usiku, DR Congo itakabiliana na Jamaica na saa 12:00 asubuhi, Iraq itacheza na Bolivia.