Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya nishati, Tanzania imeanza kushuhudia mageuzi makubwa katika sekta ya nishati jadidifu. Miongoni mwa kampuni zilizo mstari wa mbele katika mageuzi hayo ni Ensol Tanzania, ambayo imejijengea sifa ya kuwa kinara wa suluhisho za nishati safi nchini.

Kupitia mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Ensol Tanzania, Mhandisi Hamisi Mikate tumefanikiwa kufahamu kwa undani safari ya kampuni hiyo, mafanikio yake, changamoto, na dira yake ya baadaye katika kuendeleza nishati jadidifu.

Historia ya Ensol Tanzania na malengo ya kuanzishwa kwake

Akizungumzia historia ya kampuni hiyo, Mhandisi Mikate anasema kuwa kampuni ilianzishwa zaidi ya miaka 25 iliyopita ikiwa na lengo kuu la kuleta suluhisho mbadala za nishati kwa Watanzania, hasa katika maeneo ambayo hayakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Wazo la kuanzisha Ensol lilitokana na uhitaji mkubwa wa nishati vijijini na hata mijini ambapo upatikanaji wa umeme ulikuwa changamoto. Tulilenga kuleta teknolojia rahisi, nafuu na endelevu, hasa katika matumizi ya nishati ya jua,” anasema.

Anaongeza kuwa mwanzoni kampuni ilianza kwa kusambaza mifumo midogo ya sola kwa matumizi ya nyumbani, lakini kadri miaka ilivyopita, mahitaji yaliongezeka na hivyo kupanua wigo wa huduma zake.

Mafanikio na mabadiliko ndani ya miaka 25

Katika kipindi cha zaidi ya robo karne, Ensol Tanzania imepiga hatua kubwa. Kampuni imeweza kuhudumia maelfu ya wateja kote nchini, kutoka kaya binafsi hadi taasisi kubwa kama shule, hospitali, taasisi za kiserikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.

“Moja ya mafanikio makubwa ni kuweza kusambaza mifumo ya sola katika maelfu ya vijiji ambavyo hapo awali havikuwa na umeme. Pia tumeshiriki katika miradi ya kitaifa ya kusambaza nishati safi kwa jamii,” anasema Mhandisi Mikate.

Mabadiliko ya kiteknolojia yamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo. Kutoka mifumo ya msingi ya sola, sasa Ensol inatoa teknolojia za kisasa zaidi zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi nishati na kutumia kwa ufanisi.

Mitambo ya umeme wa jua ikiwa imefungwa juu ya paa za baadhi ya majengo ya biashara na ofisi Upanga, jijini Dar es Salaam.

Aidha, kampuni imewekeza katika mafunzo ya wataalamu wa ndani ili kuhakikisha huduma bora na endelevu zinapatikana kwa wateja wake.

Bidhaa na huduma zinazotolewa na Ensol Tanzania

Ensol Tanzania inatoa huduma na bidhaa mbalimbali zinazolenga kukidhi mahitaji tofauti ya nishati. Bidhaa hizo ni pamoja na: mifumo ya sola kwa matumizi ya nyumbani na biashara, pampu za maji zinazotumia nishati ya jua, taa za sola kwa matumizi ya ndani na nje, betri za kuhifadhi nishati, mifumo ya umeme kwa taasisi kama shule na hospitali.

Mbali na bidhaa, kampuni pia hutoa huduma za ushauri, usanifu wa mifumo ya nishati, usakinishaji (installation) pamoja na matengenezo. “Mteja wetu hupata suluhisho kamili kuanzia ushauri hadi utekelezaji. Tunahakikisha mfumo unaofungwa unakidhi mahitaji yake halisi,” anasisitiza Mhandisi Mikate.

Huduma hizi zimeifanya Ensol kuwa miongoni mwa kampuni zinazoaminika zaidi nchini jambo lililoiwezesha kupata kandarasi za miradi mikubwa kuanzia ya Serikali, sekta binafsi na mashirika ya maendeleo.

Kwa nini uichague Ensol kwa bidhaa na huduma za nishati jadidifu?

Katika sekta inayokua kwa kasi, ushindani ni mkubwa. Hata hivyo, Ensol Tanzania imeweza kujitofautisha kwa njia kadhaa. Ensol ni wakandarasi wabobevu (speciality contractors) waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na kupewa leseni ya daraja la kwanza (Class 1) hivyo kuiwezesha kutekeleza miradi yote ya sola.

Kingine ni ubora wa bidhaa na huduma. Kampuni inasisitiza matumizi ya vifaa vilivyothibitishwa kimataifa na vinavyodumu kwa muda mrefu. Huduma bora kwa wateja, ambapo kampuni imeweka mfumo wa ufuatiliaji ili kuhakikisha wateja wanapata msaada kwa wakati.

“Tunaamini katika kujenga uhusiano wa muda mrefu na wateja wetu. Hatuuzi tu bidhaa, bali tunatoa suluhisho endelevu,” anasema Mhandisi Mikate.

Pia, uwepo wa timu ya wataalamu wa ndani unasaidia kutoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, tofauti na baadhi ya kampuni zinazotegemea wataalamu kutoka nje.

Miradi Iliyotekelezwa na Inayoendelea

Katika miaka ya hivi karibuni, Ensol Tanzania imekuwa ikishiriki katika miradi mbalimbali yenye faida kubwa kwa jamii. Miradi hiyo inahusisha ufungaji wa taa za barabarani kwa kushirikiana na Serikali, usambazaji na ufungaji wa mifumo ya sola kwa matumizi ya nyumbani na taasisi, miradi ya maji safi kupitia pampu za sola na usambazaji wa nishati katika taasisi za elimu.

“Katika utekelezaji wa miradi hii, tunashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya maendeleo, Serikali, na sekta binafsi katika kutekeleza miradi mikubwa. Tumetekeleza miradi mikubwa ya Serikali kupitia wizara mbalimbali, mashirika ya maendeleo kama SIDA, UNDP, GIZ nk,” anaeleza Mhandisi Mikate.

Baadhi ya miradi inayoendelea ni pamoja na ufungaji wa mifumo ya sola katika shule za sekondari na vituo vya afya, ambapo umeme umesaidia kuboresha huduma za elimu na afya.

Nafasi ya Ensol katika ajenda ya nishati safi ya kupikia

Ajenda ya nishati safi ya kupikia imekuwa ikipewa kipaumbele nchini kutokana na athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati chafu. Ensol Tanzania imekuwa sehemu ya suluhisho kwa kuanzisha miradi ya majiko yanayotumia nishati safi, hasa katika shule za bweni.

“Tumeanza kusambaza majiko ya kisasa yanayotumia nishati ya sola (Solar energy Stove) ambayo yanapunguza matumizi ya kuni na mkaa. Hii inalinda mazingira na pia kuboresha afya za watumiaji,” anasema Mhandisi Mikate.

Katika shule ambazo zimefikiwa na Ensol Tanzania, majiko hayo yamepunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa upishi. Pia, wanafunzi wanapata mazingira bora zaidi ya kujifunza bila athari za moshi.

Mikakati ya baadaye ya kuboresha huduma

Ensol Tanzania ina mipango kabambe ya kuendelea kuboresha huduma zake na kupanua wigo wa shughuli zake. Miongoni mwa mikakati hiyo ni: kuongeza uwekezaji katika teknolojia mpya za nishati jadidifu, kupanua huduma katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, kuimarisha ushirikiano na wadau wa ndani na kimataifa na kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi.

“Tunataka kuona kila Mtanzania anapata nishati safi na ya uhakika. Hii si tu biashara, bali ni dhamira ya kuchangia maendeleo ya Taifa. Lakini pia kuendelea kuweka tabasamu katika nyuso za wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kama inavyosema kaulimbiu yetu ya ‘nishati kwa tabasamu’,” anasema Mhandisi Mikate.

Safari ya Ensol Tanzania ni ushahidi kuwa sekta binafsi inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nishati jadidifu nchini. Kupitia ubunifu, uwekezaji na ushirikiano, kampuni imeweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya maelfu ya Watanzania.

Kadri dunia inavyoelekea katika matumizi ya nishati safi, mchango wa kampuni kama Ensol Tanzania utakuwa muhimu zaidi katika kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya maendeleo endelevu.

Kwa sasa, matumaini ni makubwa kuwa juhudi hizi zitaendelea kuzaa matunda na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa vinara wa matumizi ya nishati jadidifu barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *