
KIUNGO wa kati wa Singida Black Stars, Ahmed Bakari ‘Pipino’ amesema siyo kitu rahisi kupata nafasi ya kucheza katikati ya mapro anaoshindana nao namba, kinachombeba ni nidhamu, bidii na kutokata tamaa kujituma mazoezini.
Mastaa wa kigeni anaocheza nao nafasi moja Pipino ni mkongwe Khalid Aucho na Emmanuel Keyekeh, jambo ambalo anasema anatakiwa kujifunza na kupambana ili kuwa na muendelezo wa kiwango.
“Napata nafasi ya kucheza pamoja na hilo, naendelea kujifunza kwa watu ambao wamenizidi uzoefu wa kucheza ligi ya hapa Tanzania na nchi walizotoka, bado nina safari ndefu ya kufanya vitu vikubwa katika kazi hii,” amesema Pipino na kuongeza;
“Mfano kati ya viungo wa kati ambao nilikuwa nawaangalia kwa kujifunza na ilikuwa ndoto zangu siku moja nicheze nao ni Aucho, ambaye tupo wote Singida, vitu ninavyofaidika naye nikujifunza ubora na kudumu kucheza kwa kiwango vinatokana na nini, jambo zuri zaidi anapenda mtu mwingine afike mbali zaidi.”
Pipino alisajiliwa na KMC dirisha dogo msimu uliyopita kutoka Kituo cha Magnet ambapo huduma yake ikawavutia Simba, Yanga na Azam FC, lakini zikagonga mwamba akatua SBS.
Kiungo huyo amekuwa akionyesha kiwango cha hali ya juu kwenye kikosi cha Singida na ni mmoja kati ya wachezaji ambao wamefanikiwa kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars wakiwa na umri mdogo.