MICHUANO ya mpira wa kikapu ya Asma Mwinyi Next Generation imefikia tamati kwa timu tatu kung’ara zikitwaa ubingwa katika rika tofauti.

Timu hizo ni Mafunzo ya wanawake umri wa miaka 18, Dream Chasers ya wavulana umri wa miaka 15 na Kwerekwe Yankees kwa wavulana miaka 18.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 20, yalianza Jumamosi Machi 28, 2026 na kumalizika Jumatatu Machi 30, 2026 kwenye uwanja wa ndani wa New Amaan Complex, Zanzibar, yalilenga kukuza vipaji vya vijana na kuibua wachezaji bora wa baadaye.

Kwa nafasi nyingine, timu ya JKU ilishika nafasi ya pili kwa wanawake chini ya miaka 18, ikifuatiwa na African Magic waliomaliza katika nafasi ya tatu. Kwa upande wa wavulana wa umri wa miaka 15, Stone Town ilimaliza nafasi ya pili huku Kwerekwe Yankees wakishika nafasi ya tatu. Kwa wavulana wa miaka 18, Dream Chasers walimaliza nafasi ya pili na Unmatched kushika nafasi ya tatu.

Mabingwa hao wa kila rika walikabidhiwa vikombe na medali na Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahma Sanya ambapo aliwapongeza washiriki kwa kuonesha ushindani na nidhamu katika mashindano hayo.

Mbali na zawadi, waandaaji walitoa tuzo maalumu kwa wachezaji bora waliofanya vizuri zaidi ambapo katika kundi la wavulana chini ya miaka 15, ilikwenda kwa Sheiff Abass wa Dream Chasers, aliyekabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo jezi, kofia, mkoba, mpira pamoja na Sh20,000.

Kwa upande wa wanawake chini ya miaka 18, tuzo ya MVP ilinyakuliwa na Zuhra Abdalla wa Mafunzo, naye alizawadiwa Sh20,000 pamoja na zawadi nyinginezo.

Katika kundi la wavulana wa miaka 18, mchezaji bora alitoka katika timu ya Kwerekwe Yankees, huku tuzo ya mchezaji mdogo zaidi katika mashindano yote ikienda kwa Ajhtar Sheha wa Stone Town, aliyevutia wengi kwa kiwango chake licha ya umri mdogo.

Mashindano ya Asma Mwinyi New Generation yameendelea kuthibitisha kuwa jukwaa muhimu la kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika mchezo wa mpira wa kikapu Zanzibar, huku wadau wakihimizwa kuendelea kuyaunga mkono ili kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *