
HABARI itakayowafanya mashabiki wa Yanga kucheka kwa furaha ni hii ya baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na Simba kuhusu kiungo, Mohammed Damaro.
Iko hivi, Simba iliwasilisha malalamiko mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji juu ya uhalali wa Damaro ikipinga usajili wa kiungo huyo kwa madai unaifanya Yanga kuwa na wachezaji 13 wa kigeni badala ya 12 wanaotakiwa kikanuni.
Taarifa iliyotolewa na TFF ilisema kamati hiyo imetupa shauri hilo la Simba ikieleza kuwa usajili wa Damaro hauna dosari kwa vile habanwi na kanuni zilizowasilishwa na klabu ya Simba.
Simba katika malalamiko yake ilidai usajili huo wa Camara ilikiuka kanuni ya 62 (1) ya Ligi Kuu pamoja na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Wakati wa kufanya maamuzi hayo, Simba iliwakilishwa na mwanasheria wa klabu hiyo, Hosea Chamba aliyeambatana na mhasibu mkuu wa timu hiyo, Seleman Kaumbu.
Kufuatia uamuzi huo bosi mmoja wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina amesema hawakwenda kusikiliza shauri hilo kutokana na kuamini kwamba lilikuwa na mrengo wa propaganda.
“Tulijua uamuzi utakuwa hivyo kwa kuwa hiyo ndio haki na usahihi. Unajua hawa wenzetu wanajua wanachokifanya. Wanataka kututoa kwenye utulivu wa kimashindano. Kiukweli hatukuwa na haja ya kuwapeleka watu wetu huko, tuliamini TFF itatoa haki kupitia kamati yake bila sisi kuwepo,” amesema bosi huyo.
Baada ya Simba kupata uamuzi huo gazeti hili linafahamu kwamba wekundu hao wanapiga hesabu za kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi Michezoni (CAS), kupinga uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.
“Hukumu imetoka muda huu, tunasubiri maamuzi ya wanasheria wetu, wakiona kama kuna haja ya kwenda mbele Simba itakwenda mpaka CAS kupata uamuzi wa mwisho,” amesema bosi huyo wa Simba ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo wakati akizungumza na Mwanaspoti.