Dar es Salaam. Serikali imezitaka taasisi na washirika wa maendeleo kuhakikisha miradi na programu wanazotekeleza nchini, zinaendana na vipaumbele vya taifa vilivyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Hatua hiyo imetajwa kuwa muhimu katika kuongeza tija ya rasilimali, kuimarisha uratibu wa miradi na kuhakikisha matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao cha majadiliano kati ya Tume ya Taifa ya Mipango na Washirika wa Maendeleo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais–Mipango, Tausi Kida amesema Serikali inalenga kuhakikisha mipango yote ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa.

Amesema Serikali ina matarajio kadhaa muhimu kutoka kwa washirika wa maendeleo, ikiwamo kuimarisha majadiliano yenye mfumo maalumu na yanayoendelea ili kuboresha uratibu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kida amesema lengo la Serikali ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania chini ya Dira 2050, kuimarisha uratibu kati ya Serikali na washirika wa maendeleo na kuhakikisha programu zote za maendeleo zinaendana na mifumo ya kitaifa ya mipango.

Wadau na washirika wa maendeleo walioshiriki kwenye kikao cha pamoja na Tume ya Mipango kilicholenga kujadili ushirika wa wadau hao katika utekelezaji Dira 2050.

“Tunataka kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu tunakokwenda kama taifa. Ni muhimu kwa kila mdau kuhakikisha juhudi zake zinaendana na malengo ya taifa ili kuongeza ufanisi na matokeo yanayopimika,” amesema.

Kida ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa Serikali na washirika wa maendeleo kubadilishana mawazo kuhusu maeneo ya ushirikiano na kukubaliana mbinu zitakazosaidia kuongeza mshikamano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema Serikali inaamini majadiliano ya mara kwa mara na yenye mfumo unaoeleweka, yataongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali na kupunguza urudiaji wa miradi.

“Tunasisitiza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara yenye mfumo unaoeleweka. Hii itasaidia kupunguza mgawanyiko wa miradi, kuongeza mshikamano wa juhudi na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa njia ya kimkakati,” amesema.

Aidha, amesema Serikali inatarajia kuendelea kupata msaada kutoka kwa washirika wa maendeleo katika kuimarisha uwezo wa taasisi za umma pamoja na kuvutia uwekezaji wenye matokeo katika sekta za kipaumbele za maendeleo.

Kwa upande mwingine, Kida amezitaka taasisi za maendeleo kutumia uzoefu wao wa kimataifa na utaalamu wa kiufundi kusaidia kuboresha mifumo ya upangaji, ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo.

Amesema hatua hiyo itasaidia kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi, kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi na kuboresha matokeo ya programu mbalimbali za maendeleo.

Pia amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Mipango inapaswa kushirikishwa mapema katika hatua zote za kubuni na kutekeleza programu za maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inaendana na mwelekeo wa kimkakati wa taifa tangu mwanzo.

Wadau na washirika wa maendeleo walioshiriki kwenye kikao cha pamoja na Tume ya Mipango kilicholenga kujadili ushirika wa wadau hao katika utekelezaji Dira 2050.

“Kwa kufanya hivyo tutaimarisha msingi wa pamoja wa utekelezaji, kupunguza urudiaji wa miradi na kuhakikisha kila juhudi inaleta mchango unaoonekana katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Kida.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, William Shelukindo amesema ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo umeendelea kuwa kichocheo muhimu katika safari ya maendeleo ya nchi.

Amesema ushirikiano huo umefika wakati muafaka ambapo Tanzania inaendelea kusonga mbele na utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ya muda mrefu.

Shelukindo amesema Serikali inaweka mkazo mkubwa kuhakikisha programu za washirika wa maendeleo zinaendana na vipaumbele vya taifa ili kuongeza ufanisi, mshikamano wa utekelezaji na matokeo endelevu kwa wananchi.

Amesema Serikali ya Tanzania inathamini kwa kiwango kikubwa ushirikiano wake wa kimkakati na washirika wa maendeleo ambao umeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo nchini.

Kwa mujibu wa takwimu alizotoa Balozi Shelukindo, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara kutokana na sera thabiti za kiuchumi na ushirikiano wa karibu na washirika wa maendeleo.

Amesema uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa kati ya asilimia 5.2 hadi 5.6 kwa mwaka, hali inayoonyesha uthabiti wa msingi wa uchumi licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani.

Aidha, amesema uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) umefikia takribani Dola za Marekani 1.3 bilioni kwa mwaka, jambo linaloashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika mazingira ya biashara nchini.

Katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, amesema kumekuwa na ongezeko la uzalishaji kutokana na upanuzi wa miradi ya umwagiliaji, kuboreshwa kwa huduma za ugani na kuimarika kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Kwa upande wa viwanda, amesema sekta ya uzalishaji imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 4 hadi 5 kila mwaka, hali inayochangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji pamoja na juhudi za kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Amesema sekta ya nishati pia inaendelea kuwa mhimili muhimu wa mabadiliko ya kiuchumi, huku uwezo wa uzalishaji wa umeme ukizidi megawati 2,500 na upatikanaji wa umeme kufikia asilimia 78 nchini, ikiwamo asilimia 65 vijijini.

Aidha, miradi mikubwa ya miundombinu kama reli ya kisasa ya SGR, upanuzi wa bandari pamoja na maboresho ya barabara na viwanja vya ndege imeendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *