Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 3
Nchi sita za mwisho zimefuzu kwa Kombe la Dunia 2026, hivyo kukamilisha orodha ya timu 48 zitakazoshiriki katika mashindano hayo.
DR Congo na Iraq zilikuwa timu za mwisho kufuzu, baada ya kujipatia fursa ya kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakalofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico kuanzia tarehe 11 Juni hadi 19 Julai.
Mchakato mrefu wa kufuzu kushiriki katika kombe hilo ulioanza Septemba mwaka 2023 sasa umekamilika, ukihusisha mashirikisho sita ya soka duniani.
Timu nne za mwisho kutoka Ulaya zilithibitishwa siku ya Jumanne, huku habari kubwa ikiwa ni kwamba mabingwa wa mara nne Italy walitolewa na BosniaHerzegovina. Jamhuri ya Czech, Uturuki na Uswidi pia zilifuzu.
DR Congo na Iraq zilipata tiketi zao baada ya ushindi dhidi ya Jamaica na Bolivia mtawalia.
Kati ya timu 48 zitakazoshiriki, nchi tatu ambazo ni wenyeji wa kombe hilo walifuzu moja kwa moja, huku nafasi 43 zikijazwa kupitia hatua za kufuzu katika mashirikisho mbalimbali, na nafasi mbili za mwisho kuamuliwa kupitia mchujo wa mabara tofauti.
Sasa, baada ya timu zote kuthibitishwa macho yanaelekezwa kwenye Kombe la Dunia.
Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yataendeshwaje?
Toleo la mwaka 2026 litakuwa kubwa zaidi kuwahi kufanyika, likiwa na jumla ya timu 48 , hii ikiwa ongezeko kutoka timu 32 zilizoshiriki Kombe la Dunia 2022. Jumla ya mechi 104 zitachezwa katika nchi tatu kwa mara ya kwanza.
Mashindano yatafanyika kati ya tarehe 11 Juni hadi 19 Julai katika miji 16, miji 11 nchini Marekani, mitatu Mexico na miwili Canada zitatumika.
Pia yatadumu kwa siku 39 ,r ikilinganishwa na siku 29 mwaka 2022 na siku 32 katika mashindano ya 2014 na 2018. Mfumo mpya wa mashindano utakuwa na makundi 12, kila kundi likiwa na timu nne.
Mechi ya ufunguzi itawakutanisha Mexico dhidi ya South Africa katika Estadio Azteca, jijini Mexico City tarehe 11 Juni siku 18 baada ya kumalizika kwa msimu wa Premier League.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi (jumla 24) pamoja na timu nane bora zilizoshika nafasi ya tatu zitasonga mbele hadi hatua ya mtoano, ambayo itaanza na hatua ya timu 32.
Bingwa mpya wa dunia atapatikana tarehe 19 Julai katika MetLife Stadium, iliyoko New Jersey.
Mechi za Kombe la Dunia 2026 zitachezwa lini?
Kutokana na mechi kufanyika katika maeneo yenye tofauti ya saa (time zones) nne na umbali wa hadi maili 2,800 kati ya viwanja, kutakuwa na jumla ya saa 13 tofauti za kuanza kwa mechi.
Hii ina maana kwa watazamaji wa Ulaya, baadhi ya mechi zitachezwa kuanzia saa sita usiku na kuendelea.
Kwa mfano, mechi zote tano za hatua ya makundi zitakazochezwa katika Kansas City zitakuwa usiku wa manane kwa saa za Uingereza. Mechi ya mapema zaidi itaanza saa 00:00 BST Ijumaa, tarehe 26 Juni kati ya Tunisia dhidi ya Netherlands, huku ya mwisho ikiwa saa 03:00 BST kati ya Algeria na Austria Jumapili, tarehe 28 Juni.
Eneo la San Francisco Bay Area litakuwa mwenyeji wa mechi mbili zitakazoanza saa 05:00 BST: Austria dhidi ya Jordan Jumanne, tarehe 16 Juni na Turkey dhidi ya Paraguay Ijumaa, tarehe 19 Juni.
Pia kutakuwa na mechi za saa 05:00 BST katika Vancouver — Australia dhidi ya Turkey Jumamosi, tarehe 13 Juni — na katika Guadalupe, Tunisia watakapocheza dhidi ya Japan Jumamosi, tarehe 20 Juni.
Kwa jumla, kutakuwa na mechi 35 za hatua ya makundi zitakazoanza kati ya saa 00:00 BST hadi 05:00 BST — karibu nusu ya mechi zote 72 za hatua hiyo.
Hata hivyo, muda unaotumika zaidi kuanza mechi ni saa 20:00 BST, ambapo mechi 12 za hatua ya makundi zitachezwa wakati huo.