
MAKAMU Mwenyekiti mpya wa Barberian FC, Robert Munis amesema baada ya kukabidhiwa wadhifa huo muhimu kikosini humo, kwa sasa kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha anainusuru timu hiyo isishuke daraja msimu huu, licha ya ushindani uliopo.
Munis, aliyewahi kushika wadhifa huo wa makamu mwenyekiti akiwa na kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania, alijiunga na Barberian FC zamani Kiluvya United, huku akiahidi kuipambania isishuke daraja, licha ya timu hiyo kuburuza mkiani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Munis amesema “Nimeichukua timu ikiwa katika hali mbaya sana kwa sababu mwenendo wetu siyo mzuri na nafasi tuliyopo tunahitaji kufanya kazi ya ziada kwa mechi zilizobakia, bado tunaweza kufikia malengo yetu tukiendeleza mshikamano wetu,” amesema Munis.
Munis, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na Mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema baada ya ligi kusimama wamekuwa pia na vikao vya kujadili mustakabali wao.
“Mapumziko haya kwetu yamekuwa na faida kwa sababu yametupa muda wa kukaa na benchi la ufundi na wachezaji na kuangalia ni kwa namna gani mechi tisa zilizobakia tunafanya vizuri, kiukweli hadi sasa tuko katika mstari mzuri,” amesema Munis.
Barberian inanyemelea rekodi mbovu msimu huu katika Ligi ya Championship, baada ya kikosi hicho kushinda mechi moja tu hadi sasa kati ya 21 ilizocheza, ikiwa mkiani.
Katika mechi hiyo moja ilishinda mabao 2-1, dhidi ya TMA FC kutoka jijini, Arusha, Januari 11, 2026, ila, baada ya hapo imetoka sare saba na kuchapwa 13, ikiwa nafasi ya 16 na pointi 10.
Kwa misimu ya hivi karibuni, timu iliyoshinda mechi chache katika Ligi ya Championship, ni Ruvu Shooting, msimu wa 2023-2024 na ilishinda mbili, sare saba na kuchapwa 21, ikiwa nafasi ya 16 na pointi 13.