
MKUU wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), Said Shamhuna amesema baada ya kuona timu ya wanawake inafanya vizuri kwa kuchukua ubingwa mara kwa mara, wamevutiwa na kuhitaji kutoa fursa hiyo kwa wanaume.
Amesema, kabla ya kuanza kwa wakubwa, wameamua kuwekeza kwa vijana wadogo ili kuona mwamko wao na amevutiwa kuona vipaji vinavyostahili kutunzwa na kukuzwa.
“Kwenye kikosi changu sina timu ya mpira wa kikapu ya wanaume, ipo ya wanawake ambayo inafanya vizuri, hivyo nahitaji kuwekeza kwenye mchezo huu kwa wanaume kwani nimevutiwa sana,” amesema.
Mkuu huyo amesema huu ni wakati sahihi wa KVZ kuanzisha timu hiyo kwani vipaji vipo, hivyo mashabiki wa mchezo huo wasubirie mazuri kutoka kwao.
Shamhuna ni miongoni mwa viongozi wanaohuisha na kuwekeza zaidi kwenye michezo ikiwemo mpira wa miguu, netiboli na kikapu upande wa wanawake na sasa kwa wanaume.
Pia, mkuu huyo amesema baada kufanikiwa kwenye ulinzi na usalama wa kikosi hicho, kwa sasa anahitaji kuiweka KVZ kwenye ramani ya michezo na kuhakikisha kila mchezo aliouanzisha unafanya vizuri ikiwemo kutoa wachezaji kucheza Ligi Kuu Bara.