
LICHA ya Raskazone inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Sharpboys, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Haji Kombo Haji amelia na baadhi ya wachezaji kuchelewa kufika kwenye uwanja wa mazoezi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo amesema kati ya vitu vinavyompa changamoto na ambavyo angependa wachezaji wake kubadilika kabla ya msimu kumalizika ni kuacha tabia ya uchelewaji.
“Nachukizwa na wachezaji kuchelewa kuripoti kwenye uwanja wa mazoezi kwa wakati uliopangwa, kiuhalisia wanatupa kazi kubwa walimu wao,” amesema.
Timu hiyo imeendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupanda daraja kushiriki Ligi Kuu Zanzibar msimu ujao baada ya kukusanya pointi 52 kwenye mechi 21, huku ikiwa na tofauti ya alama nne na kinara wa ligi hiyo Black Sailor yenye pointi 56.
Kocha Haji amesema timu hiyo imejinoa vizuri na ina uwezo wa kupambana kubaki kwenye ligi kwa misimu miwili hadi mitatu kwani ina uwezo wa kucheza na timu ya aina yoyote na kupata matokeo mazuri.
Amesema, hiyo inachangiwa na kikosi chake kuwa na muunganiko mzuri na wakati wote wanajiandaa kwa ajili ya kufanya vizuri na sio kuwa wasindikizaji wa ligi.
Hivyo, amesema endapo timu hiyo itapanda Ligi Kuu inaahidi kutoa ushindani wa kutosha kwa timu pinzani kwa sababu inajiandaa na hilo.
Pia, amesema kabla ya mechi anawandaa wachezaji kisaikolojia kwa kuwapata morali, lengo likiwa ni kupambana hata kwa kipindi kigumu cha mchezo.
“Mbinu ambayo natumia kukiendeleza kikosi na kutoa matokeo mazuri ni kuwapa hamasa wachezaji na hakuna ambaye nina mdharau, wote ni wanangu tupo kwa ajili ya kufanyakazi,” amesema.
Timu hiyo iliibuka na ushindi dhidi ya Sharp Boys kwenye mzunguko wa 21 kwenye Uwanja wa Tazari, mechi iliyokuwa na ushindani mkali na kuvutia mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia.
Kwa upande wa Kundemba, imefikisha pointi 38 ikishika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, huku Urafiki ikiwa nafasi ya 10 ikikusanya pointi 24, Sebleni nafasi ya nne na pointi 33, wakati Sharp Boys inashika nafasi ya 15 kwa pointi 14.