Dar es Salaam. Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikipambana na muuaji wa kimya kimya bila mafanikio huku familia nyingi zikipoteza kiungo muhimu cha familia, ambacho ni mama.

Muuaji huyo wa kimya kimya si mwingine bali ni vifo vya uzazi kwa kinamama, ambavyo vinaitwa muuaji wa kimya kimya kwa sababu tu, wengi hawaoni kama vifo hivyo ni janga na ni vifo vinavyoumiza, kwani vinatokea pindi mwanamke anapoleta uhai duniani.

Laiti ingekuwa  ni  basi la abiria kila linapokwenda katika safari zake linapata ajali na kuua watu wawili kila siku, basi hilo lingetazamwa kama janga kubwa kwa taifa na maswali mengi angehojiwa dereva na mmiliki wa basi.

Takwimu kutoka cha Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (CDC-Afrika) zinaonyesha kuwa, vifo vya uzazi Tanzania vimepungua kwa asilimia 80 kutoka 556 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

Katika mgawanyo wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000, kwa mwaka ni sawa na vifo viwili kila siku vinavyotokana na uzazi kwa kinamama.Na hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuamua kulivalia njuga suala la vifo vya uzazi kwa kinamama.

Hali ilivyo Hospitakli ya Mwananyamala

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Irene Barongo, vifo vya uzazi kwa kinamama vilikuwa saba katika mwaka wa fedha, 2023/2024 na mwaka jana, kulikuwa na vifo vitatu tu.

“Kuna mengi yamefanywa, kwa kupitia ‘Mama Samia Sponsorship’ madaktari bingwa wamesomeshwa ambao wanarudi katika hospitali, hali ambayo imechangia kupunguza vifo vya uzazi kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Kwa upande wa watoto, hospitali hiyo imepunguza vifo vya watoto. Daktari bingwa wa watoto, Makena Kato anasema, awali walikuwa wakitegemea vifaa vya kupumulia kwa watoto wenye changamoto kupumua(sipap).

Anasema, awali walikuwa wakitegemea ‘sipap’ moja tu lakini sasa Serikali imeongeza mashine zaidi ya 20.

“Kwa mfano mtoto amezaliwa na changamoto ya upumuaji labda kwa sababu alizaliwa kabla ya wakati au njiti, halafu hospitali ina sipap moja, basi hapo ni kupanga foleni, kusubiri mtoto aliyewekwa atoke. Kwa hali ile ni rahisi watoto kufariki.” Anasema.

Lakini Dk Kanto anaongelea umuhimu wa afya na uhai wa mama wakati wa kujifungua na kusema, Mungu amemuumba mwanamke kwa namna ya kipekee ili alete uhai duniani, hivyo kupoteza maisha wakati wa kitendo hicho si haki.

Dk Barongo anafafanua zaidi jinsi ambavyo Mwananyamala wameingilia kati vifo vya uzazi kwa kinamama na kusema kampeni kubwa imefanyika katika suala la kukusanya damu salama, jambo ambalo limepunguza vifo vya uzazi.

Anasema kwa mwaka hospitali inazalisha wanawake kuanzia 5,000 mpaka 6000, na vifo vinavyotokea kwa kiasi kikubwa havisababishwi na ukosefu wa damu.

Akiuzungumzia mwezi wa maadhimisho ya wanawake duniani, Dk Barongo anasema, hakuna jambo gumu kama pale ambapo mjamzito anajifungua na kisha anafariki dunia na kumuacha mtoto.

“Lazima ndani ya saa 24, lazima tukae, tuitane, tuulizane nini kimetokea, tunaiita ‘mortality review’ tunaangalia tumekosea wapi. Cha muhimu kusiwepo na vifo vya wanawake wakati wa uzazi, kwa sababu mama kama kiumbe anayeleta uhai duniani, hastahili kufa”anasema na kuongeza:

“Kikitokea kifo cha mwanamke wakati wa kujifungua na akabaki mtoto salama, tunajiuliza maswali mengi, huyu mtoto atabaki na nani, atanyonya nini? Atalelewa na nani? Ni vifo vinavyoumiza sana”

Dk Barongo anasema katika kupunguza vifo vya uzazi hata wauguzi na madaktari, wanasimamiwa katika kubadili mitazamo na kuondoa lugha chafu kwa wagonjwa wakiwamo wajawazito.

Anaongeza kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan alilibeba suala la afya ya uzazi kwa kinamama kama mama akitambua nafasi ya uzazi kwenye jamii.

“Kwa kweli katika awamu hii tumeona, yule ni mama na ninavyoona katika uongozi wake ameamua kumuangalia mama na mtoto, na kiuhalisia katika uwekezaji uliowekwa kwenye sekta ya afya, hakuna kifaa ambacho tutakiomba tukanyimwa na hiyo imesaidia sana kupunguza vifo vya kinamama,” anasema na kuongeza:

‘Kila mahali mama Samia amewekeza kwenye afya ya mama na mtoto, kwa kweli kama ni kutajwa kuwa kinara wa afya ya mama na mtoto anastahili.”

Malengo ya Maendeleo Endelevu(SDG) yanataka nchi za Afrika kupunguza vifo vya uzazi hadi kufikia 70 katika kila vizazi hai 100,000. Lakini Tanzania bado haijafikia lengo hilo ingawa jitihada za dhati na matokeo yameonekana kwa asilimia 80.

Hospitali ya Amana

Mkunga mbobezi, Joyce Njenga wa Hospitali ya Rufaa ya Amana anasema, miaka mitano iliyopita, Amana ilikuwa ina idadi kubwa ya vifo vya uzazi kwa kinamama, kwa mfano mwaka 2023, kinamama 12 walifariki kwa mwaka kwa sababu ya uzazi na mpaka mwaka jana kulikuwa na vifo viwili tu.

“Hii inatokana na kuongezwa kwa vifaa tiba ikiwamo machine ya ‘ultrasound’ kingine ni ushirikiano katika kufanya kazi, akifika tu anaangaliwa anahitaji huduma gani, kwa wanaohitaji upasuaji, ndani ya nusu saa anaandaliwa na kupelekwa chumba cha upasuaji” anasema

Anasema Amana kuna madaktari bingwa wa nane wa masuala ya uzazi na wakunga wabobezi watatu.

“Zamani mkunga mmoja alizalisha watoto sita hadi saba peke yake, sasa hivi huduma za afya zimeimarishwa zaidi katika hospitali za pembezoni na kusaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa katika hospitali za rufaa” anasema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk Bryson Kiwale anasema vifo 556 ni sawa na mabasi kadhaa ya abiria yaanguke kisha yasababishe vifo.

Anasema, kama mabasi hayo yangeanguka na kuua, pengine ungetangazwa msiba mzito kwa taifa lakini kwa sababu ni msiba unaoikuta familia moja, na sehemu nyingine familia moja, watu hawaoni ukubwa wa vifo hivi.

“Ni dhamira ya kweli ya Serikali na wala hakuna muujiza, Serikali imeamua kuwekeza katika afya ya msingi, ikiwamo mafunzo na utayari wa watoa huduma katika sekta ya afya,” anasema

Naye Daktari bingwa wa watoto, Hospitali ya Amana, Grace Mhando, anasema ingawa vifo vya watoto bado ni changamoto kwa sasa vimepungua.

Anasema kwa sasa Tanzania inazungumzia vifo vya watoto 24 katika kila vizazi hai 1000 hali ambayo bado tunaweza kusema bado hatujafikia lengo la kidunia la kupunguza vifo hivyo hadi kufikia 12 katika kila vizazi hai 1000.

“Lakini tumeona juhudi za Serikali, kwa kupitia ‘Mama Samia Sponsorship’ madaktari bingwa wanaendea mpaka vijijini kuwahudumia watoto ambao wana hali ya chini.

Ripoti iliyochapishwa Januari mwaka 2025 na Jarida la Afya la Uingereza, imeonyesha kuwa program zilizofanyika zikihusisha serikali, taasisi za afya na wataalamu wa afya, zimewezesha kupunguza kwa asilimia 75 vifo vya uzazi katika kipindi cha miaka mitatu.

Matokeo ya utafiti huo ulifanywa katika vituo 30 vya afya vinavyopokea wagonjwa wengi nchini, yalibainisha kuwa maelfu ya kinamama waliepuka vifo vya uzazi kwa kutumia program zilizowekwa na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.

Februari mwaka jana, Taasisi ya Gates, ilimpa Rais Samia Suluhu tuzo maalum ya Goalkeepers ya kutambua mchango wake katika kuboresha afya ya mama na mtoto na lishe. Rais aliitoa tuzo hiyo kwa wafanyakazi wote wa sekta ya afya kwa mchango wao katika kupunguza vifo hivyo.

Kilichofanyika Muhimbili

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ina jukumu muhimu katika kuhakikisha kila mama anapata huduma salama ya uzazi kupitia mfumo wa kitaifa wa afya unaohusisha vituo vya ngazi zote.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Redemta Matindi, hospitali hiyo inafanya mapitio ya kina ya kila kifo cha mama mjamzito kinapotokea, ili kubaini sababu na kujifunza njia za kuzuia matukio kama hayo katika siku zijazo.

Mbali na mapitio hayo, Muhimbili inashirikiana na hospitali za rufaa za mikoa na wilaya pamoja na vituo vya afya vya ngazi za chini, kuhakikisha maboresho katika huduma za uzazi yanapatikana mapema.

Maboresho haya yamejumuisha uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya, usambazaji wa vifaa tiba muhimu, na upatikanaji wa huduma za dharura za uzazi, upasuaji, pamoja na uangalizi maalumu kwa watoto waliozaliwa na uzito mdogo.

“Muhimbili tumeweka mkazo katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya, hasa wakunga na wauguzi, kupitia mafunzo ya mara kwa mara na programu za mtandao.

“Mafunzo haya yanalenga jinsi ya kukabiliana na changamoto za dharura wakati wa kujifungua, na pale kifo kinapotokea, madaktari bingwa kutoka Muhimbili, hufanya uchambuzi wa kitaalamu ili kutoa maelekezo ya kuboresha huduma,” anafafanua Matindi.

Hata hivyo, anasema mfumo wa rufaa unakabiliwa na changamoto zinazohusiana na miundombinu ya barabara na msongamano wa magari, jambo linaloweza kuchelewesha mama kufika hospitali kwa wakati.

“Ili kupunguza hatari hiyo, vituo vya afya vinapokutana na changamoto kubwa za kitabibu vinaweza kuwasiliana moja kwa moja na madaktari bingwa wa Muhimbili kwa njia ya simu kupata ushauri wa haraka kabla ya mgonjwa kufika,” anasema.

Matindi anasema kwa jitihada hizi, takwimu zinaonyesha mafanikio makubwa. Kutoka vifo 556 vya wajawazito mwaka 2019, idadi hiyo imepungua hadi vifo 104 mwaka 2023.

Lengo la taifa ni kupunguza vifo vya wajawazito hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, na Muhimbili ikishirikiana na sekta mbalimbali, inahakikisha kila mama anapata huduma salama ya uzazi huku jamii ikipatiwa elimu ya hatari za uzazi na kuendeleza uwiano kati ya tamaduni na tiba ya kisasa.

Kwa mujibu wa madaktari katika hospitali hizi, juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi zimefanikiwa lakini bado malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) ya kufikisha vifo 70 katika kila vizazi hai 100,000 hayajafikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *