Shinyanga. Katika oparesheni ya Machi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata watuhumiwa 35 wa wizi wa vifaa vya SGR katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, pamoja na kukamata jumla ya makosa 5,648 ya barabarani.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Aprili 4, 2026 katika Ofisi ya Polisi ya Mkoa, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema kuwa watuhumiwa wote wako mikononi mwa polisi kwa uchunguzi zaidi.

“Watuhumiwa 35 wanashikiliwa kwa wizi wa vifaa vya SGR ambavyo ni vipande vya nondo 306, mabomba 32 yenye ukubwa wa mm 12, stendi za makarasha 12 na mabomba ya mraba 65 katika eneo la Msalala, na watuhumiwa wote wako mikononi mwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Magomi.

Pia ameongeza kuwa, “Jumla ya makosa 5,648 yamekamatwa, ambapo makosa ya magari ni 4,044 na makosa 1,604 ya bajaji na pikipiki, ambapo wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo,” ameongeza Magomi.

Mkazi wa Kata ya Mjini, Manispaa ya Shinyanga, Alex John ameeleza kuwa matukio ya wizi yanaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji wa ndani na nje, kwani yanaonyesha udhaifu katika ulinzi wa miradi mikubwa.

“Hii inaweza kuathiri uwekezaji mwingine muhimu wa miundombinu nchini kwa sababu za kiulinzi na kiusalama wa miradi inayotekelezwa. Nashukuru Jeshi la Polisi kwa kuwakamata watu hao, kwani wanarudisha maendeleo nyuma,” amesema John.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *