
Dar es Salaam. Mwili wa Athumani Nyanza umekabidhiwa kwa familia yake, siku 47 tangu ulipofukuliwa kutoka shimo alilokuwa amefukiwa kando ya nyumba yake, umezikwa rasmi leo.
Nyanza, anayedaiwa kuuawa na mpenzi wake kabla ya mwili wake kufukiwa mbele ya nyumba yake iliyopo Mtaa wa Kimya Kimya, Kata ya Zingiziwa, Chanika jijini Dar es Salaam, amezikwa leo Jumamosi, Aprili 4, 2026 wilayani Kisarawe, mkoani Pwani.
Mwili huo uliofukiwa kwa lengo la kuficha uhalisia wa tukio hilo, ulifukuliwa Machi 16, 2026 na Jeshi la Polisi, huku ndugu wakiahidiwa kukabidhiwa baada ya kupatikana majibu ya vinasaba (DNA) ndani ya saa 24 hadi 48, tangu sampuli kupelekwa kwa Mkemia Mkuu.
Hata hivyo, mwili huo umechukua muda mrefu kabla ya kukabidhiwa jana Ijumaa Aprili 3, 2026 kwa familia kupitia kwa baba mdogo wa marehemu, Omary Nyanza, ambaye amesema maandalizi ya mazishi yanaendelea na marehemu angezikwa leo Kisarawe.
Mdogo wa marehemu, Simba Nyanza akizungumza akiwa nyumbani kwa marehemu Chanika ambako shughuli za msiba zilifanyika, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapatia mwili wa ndugu yao.
“Tunaomba ushirikiano na wadau wote tangu kutokea kwa tukio hili, hadi tunaenda kumpuzisha ndugu yetu lakini kama familia tunawashukuru majirani,”amesema.
Pia kwa kuwa marehemu alikuwa msanii amewashukuru wasanii kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza ndugu yao katika safari yake ya mwisho pamoja na serikali kwa kuwa nao kitu kimoja.
Awali, Akizungumza kuhusu tukio hilo, Machi 20, 2026, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 18, 2026 mkoani Morogoro kufuatia uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na wananchi.
Mmoja wao alitambuliwa kwa jina la Rehema Maulid (42), mkazi wa Kigamboni laki ni jina la mtuhumiwa wa pili halikutajwa kwa sababu za kiushahidi.
Kamanda Muliro hakupatikana leo Jumamosi Aprili 4 kuzungumzia kinachoendelea baada ya mwili huo kuchunguzwa.
Machi 19, 2026, Mwananchi ilizungumza na rafiki wa marehemu, Madebe Lidai aliyekuwa anafanya naye kazi, alidai mpenzi wa Nyanza aliwekwa chini ya ulinzi kufuatia kuibuka kwa wasiwasi baada ya kutoweka kwa marehemu.
Kwa mujibu wa Lidai, mwanamke huyo alihojiwa na polisi kuhusu alipo Nyanza, lakini hakutoa majibu ya kuridhisha.
Alidai mtuhumiwa alikuwa akizima simu yake mara kwa mara, hali iliyoongeza mashaka na kuchochea uchunguzi wa kina dhidi yake.
Lidai alisema kabla ya kutoweka, marehemu alimuarifu kuwa anakwenda kumtembelea mpenzi wake Kigamboni, jambo lililomfanya aanze kumtilia shaka mwanamke huyo baada ya kupotea kwake.
Alidai hata alipofikishwa Kituo cha Polisi Chanika kwa mahojiano, mtuhumiwa alikuwa anatoa majibu yanayokinzana na wakati mwingine kuomba aachiwe ili akamtafute mpenzi wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtuhumiwa aliachiwa kwa dhamana ili kuruhusu uchunguzi kuendelea, huku akitakiwa kushirikiana na polisi katika jitihada za kumtafuta Nyanza.
Hata hivyo, hatua ya kuachiwa kwa dhamana ilizua maswali kwa familia ya marehemu kutokana na uzito wa tukio hilo.
“Sikuelewa mantiki ya kumwachia mtu katika mazingira kama haya, lakini nilihisi huenda kulikuwa na sababu za kiupelelezi,” alisema Lidai.
Baada ya kuachiwa, mtuhumiwa hakurejea wala kuonekana tena, jambo lililoongeza wasiwasi. Alidai hata mdhamini wake hakuwa akipatikana kwa urahisi wala kutoa taarifa za alipo mtuhumiwa.
Kutokana na hali hiyo, polisi waliendelea na uchunguzi, ambapo mdhamini alikamatwa kwa kufuatilia mawasiliano yake, huku juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zikiendelea, hadi alipokamatwa akiwa Morogoro.