LIMA, PERUL: KATIKA hali ya kushanga lililokuwa tukio la “kupeperusha bendera” ya Klabu ya Alianza Lima kabla ya mechi ya dabi  ya Peru dhidi ya Universitario de Deportes lilimalizika kwa kifo cha angalau mtu mmoja na majeruhi 47, jana.

Alianza Lima inayoongoza Ligi Kuu Peru (Liga 1) kwa pointi 20 ina mashabiki ‘vichaa’ ambao wanaogopewa nchini humo. Universitario de Deportes inashika nafasi ya nafasi ya nne na pointi 15.

Tukio hilo lilitokea ndani ya uwanja wa timu hiyo kwa sababu ambazo bado hazijajulikana, ingawa kuna uwezekano wa msongamano mkubwa wa watu uliosababishwa na kukanyagana.

Awali, mamlaka za Peru zilikuwa zimeripoti kuwa kulikuwa na majeruhi wengi kutokana na kuanguka kwa ukuta au eneo fulani katika Uwanja wa Alianza Lima, lakini baadaye taarifa hizo zilikanushwa baada ya kubainika kuwa miundombinu ya uwanja haikuathirika.

Mkusanyiko ulikuwa mkubwa katika jukwaa la kusini la uwanja, ambako mashabiki sugu wa Alianza Lima hukaa na inaaminika kulikuwa na idadi kubwa kupita kiasi ya watu pamoja na uwezekano wa kuzuka kwa ugomvi kati yao.

Katika video zilizosambazwa mitandaoni umati mkubwa wa watu unaonekana ukiingia katika jukwaa hilo ambalo tayari lilikuwa limejaa na muda mfupi baadaye vilisikika vilio huku watu wakijaribu kupanda juu ya migongo ya wenzao, wakiwemo watoto waliokuwa kwenye umati huo.

Kutokana na msongamano mtu mmoja alifariki dunia kutokana na ukosefu wa hewa, huku wengine wengi wakipoteza fahamu kwa kuanguka. Halmashauri ya Jiji la Lima na Manispaa ya La Victoria ambako uwanja huo upo, zilisema katika taarifa tofauti kuwa tukio la “kupeperusha bendera” halikuwa na vibali wala dhamana za usalama.

Klabu ya Alianza Lima, ambayo ni maarufu zaidi nchini Peru, ilielezea masikitiko yake na kusema kuwa, “kuanzia mwanzo, taratibu za usalama na huduma za dharura zilianzishwa mara moja, na msaada ulitolewa kwa wakati kwa walioathirika na familia zao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *