KATIKA dakika 630 alizocheza mshambuliaji wa Mbeya City, Matheo Antony amefunga mabao mawili, lakini pamoja na hilo amesema haujawa msimu mzuri kwake kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Tangu Antony ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea JKT Tanzania ambako msimu wa 2023/24 alifunga mabao manne na uliofuata (2024/25) hakuwa na mabao sababu ikiwa muda mwingi alikaa nje akiwa anauguza majeraha, amesema anatamani msimu huu kufanya makubwa.

Katika msimu huu Antony anatajwa miongoni mwa wachezaji wenye mabao mengi, lakini haoni kama linakwenda kutimia.

Mshambuliaji huyo ambaye katika mechi saba kila moja kacheza dakika 90 (ikiwa ni jumla ya dakika 630) alisema: “Sipati sana nafasi, lakini najipa moyo kwani bado mechi zipo nyingi mbele yangu. Nilitamani nimalize msimu nikiwa na mabao mengi, lakini ngoja tuone huko mbele itakuwaje.”

Matamanio yake msimu huu ni kuvunja rekodi ya mabao tisa na asisti nne aliyofunga wakati anachezea KMC msimu wa 2022/23 au kuifikia.

“Mimi ni mpambanaji siyo rahisi kukata tamaa. Nakumbuka niliwahi kukwambia huko nyuma nilifanya kazi za ukonda wa daladala, najua maisha yanahitaji moyo mgumu. Natambua ushindani ni mkali, jambo la msingi nitaendelea kupambana,” alisema Antony aliyewahi kuichezea Yanga kipindi cha nyuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *