Simanjiro. Diwani wa Kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga (Mardadi) ameingilia kati uongezaji holela wa nauli kwa baadhi ya magari ya kubeba abiria.

Mardadi akizungumza leo Jumamosi Aprili 4, 2026 amesema amepata malalamiko ya baadhi ya wenye mabasi ya wafanyabiashara ya kubebea abiria wanapandisha nauli kiholela.

Amesema hivi karibuni baadhi ya wenye magari hao walipandisha nauli ya kutoka katika kata hiyo hadi Arusha umbali wa kilomita 120 hadi 130 bila kuwashirikisha wadau.

“Mwishoni mwa mwaka jana waliongeza nauli wakilalamikia bei ya mafuta kupanda, ilipoteremka hawakushusha, sasa hivi mafuta yamepanda nao wanapandisha tena nauli bila utaratibu,” amesema Mardadi.

Amesema ameshafikisha suala hilo kwa Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani na Maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ili kukomesha hayo.

Mkazi wa Kata ya Loiborsiret, Ole Penina amesema dukuduku lake ni baadhi ya magari ya kubeba abiria kupandisha nauli kiholela hivyo viongozi wasaidie hilo.

“Viongozi tunaomba waangalie hali ya usafiri haiwezekani sasa hivi nauli imepanda kutoka Sh12,000 hadi Sh15,000 mpaka Sh20,000 je hili ni sahihi kwa kilometer 120 kutoka Arusha hadi Narakauo, Loiborsiret na Sukuro kisha kilomita 130 Sh30,000 hadi Kimotorok.”

Amewaomba viongozi wa serikali kuingilia kati na kuchukua hatua kwani tabia ya kuongeza nauli kiholela imekuwa inaota mizizi kila wakati hivyo hatua zichukuliwe.

“Naombeni mtafute kikao cha wadau wote wa sekta ya usafirishaji, mjadili kutopandisha nauli kwa kigezo cha kupanda kwa bei za mafuta na badala yake wafuate utaratibu utakaowekwa,” amesema.

Amesema wasafirishaji wanapaswa kujua kuwa hata bei hizo mpya zinawaumiza jamii na hivyo nao wawe na huruma nao siyo kukimbilia kupandisha bei ya nauli bila mpangilio.

Mwakilishi Latra Mkoa wa Manyara, Robert Matheus amesema changamoto hiyo ameshaipokea na wanaifanyia kazi.

Matheus amesema ameshawasiliana na polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani ili wachukue hatua kwa kuwapiga faini au kuwafutia leseni wanaopandisha nauli kiholela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *