WAKATI matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, walipotangaza kumsajili kipa Issa Fofana, raia wa Ivory Coast, katika dirisha kubwa la usajili la msimu huu, baadhi ya mashabiki walijua wamepata suluhisho la kudumu golini.

Na hilo ni baada ya kipa huyo, aliyezaliwa Januari 30, 2004, kuwa na msimu bora akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Fofana alitua Chamazi akitokea Al Hilal, klabu ambayo alikuwa akitawala kama mfalme golini chini ya kocha Florent Ibenge.

Matarajio yalikuwa makubwa. Sababu ya kwanza ni kuwa kipa huyo alikuwa chaguo la kwanza la Ibenge wakati wakiwa Sudan, na kocha huyo ndiye aliyependekeza asajiliwe Azam, akiamini katika umbo lake na sifa nyingine za kipekee ambazo mkongomani huyo anazihitaji kwa kipa.

Lakini miezi michache tangu kuanza kwa msimu, picha imebadilika na Fofana sasa anajikuta katika wakati mgumu ambao hakuutarajia.

KIKOSI CHA KWANZA MPAKA MBAO NDEFU

Ni jambo la kushangaza kuona mchezaji aliyesajiliwa kwa sifa kubwa na kocha anayemjua vizuri akishindwa kupata nafasi ya kuanza kikosini.

Lakini, si jambo la kushangaza sana kwa sababu hata baadhi ya klabu kama Simba na Yanga ziliwahi kusajili nyota waliovuma huko walikotoka, lakini tangu walipofika Tanzania walishindwa kutamba.

Baadhi yao ni Augustine Okejepha, alisajiliwa Simba Julai 6, 2024, akitokea Rivers United ya kwao Nigeria ambako alionyesha kiwango bora, akiibuka mchezaji bora wa ligi hiyo msimu wa 2023/24.

Mwingine ni kiungo Mousa Balla Conte, raia wa Guinea, aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea CS Sfaxien ya Tunisia. Usajili wake uliwafanya vigogo Simba na Yanga kuwania saini yake, lakini mwisho wa siku Wananchi wakaiwahi saini yake na hakudumu, akatimkia Raja Casablanca.

Sasa tangu Fofana alipojiunga na Azam, ameendelea kula mbao ndefu. Hii inashangaza zaidi kwa sababu kocha anayemweka benchi ni yule yule Ibenge aliyekuwa akimpa nafasi ya kikosi cha kwanza Al Hilal.

TAKWIMU ZAKE

Azam imeshacheza mechi 16 za Ligi Kuu, lakini kipa huyo amecheza mechi tatu tu. Hata zile za Kombe la FA bado hapati nafasi ya kuanza.

Alicheza dhidi ya Mbeya City, Azam ikiondoka na ushindi wa mabao 2-0; mechi nyingine dhidi ya JKT Tanzania na Namungo, matajiri hao wakiondoka na sare ya 1-1.

Hii ina maana kuwa amekosa zaidi ya asilimia 80 ya mechi za timu hiyo, jambo ambalo linaonekana kama pigo kwa kipa aliyekuwa na muendelezo mzuri wa mechi za Afrika.

SABABU MANULA, FOBA

Swali ambalo baadhi ya wadau wanajiuliza ni nini kimemsibu Fofana? Jibu lipo kwenye ubora wa makipa wazawa ambao wameamua kuonyesha kuwa wanaweza kudumu vizuri katika nafasi hiyo.

Nafasi ya Fofana imeangukia mikononi mwa Aishi Manula na Zuberi Foba, ambao wamekuwa wakipokezana kulilinda lango la Azam kwa mafanikio makubwa.

Manula, mwenye uzoefu wa miaka mingi kwenye ligi na timu ya taifa, amerejea kwenye kiwango chake bora na kumfanya Ibenge ashindwe kumwacha nje.

Hadi sasa Manula amecheza mechi saba kati ya 16 zilizochezwa na timu hiyo, takwimu nzuri kwa kipa ambaye alikaa nje muda mrefu akiuguza majeraha.

Kwa upande mwingine, kijana Foba amekuwa akionyesha ukomavu kila anapopewa nafasi, jambo ambalo limemfanya Fofana abaki benchi.

UBORA ULIPOTEA?

Katika mechi tatu pekee ambazo Fofana amepata nafasi ya kuanza dakika zote 90, matokeo yamekuwa ya wastani. Aliiongoza Azam kushinda 2-0 dhidi ya Mbeya City, lakini alijikuta akiambulia sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Namungo.

Ingawa hajapoteza mechi, sare hizo zimechangia kumfanya kocha aone kuwa makipa wazawa, Manula na Foba, wana utulivu zaidi na kuelewana vizuri na mabeki wao.

Hali imekuwa mbaya zaidi katika michuano ya kimataifa. Wakati Azam inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo walimaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi B wakiwa na pointi tisa, Fofana hakupata hata dakika moja ya kucheza.

Wakati akiwa Al Hilal ndiye kipa aliyekuwa na nafasi kubwa ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuisaidia timu hiyo. Hii ni ishara kuwa Ibenge anaamini kwenye ubora wa mchezaji, haijalishi amefanya kazi naye kipindi gani.

SOMO HILI HAPA

Hali ya Fofana inatoa somo kwa wachezaji wa kigeni wanaokuja nchini wakidhani kuwa watapata nafasi kirahisi. Ligi Kuu ya Tanzania kwa sasa imekua, na makipa wazawa wameongeza umakini.

Fofana alikuja akiwa na wasifu mkubwa, lakini amekutana na ukuta wa Manula na Foba ambao hawako tayari kuachia namba. Ni mtihani kwa Fofana kurejesha imani kwa Ibenge. Ikiwa atashindwa kuonyesha ushindani kwa makipa wazawa katika mechi zilizosalia, huenda ukawa msimu wake wa mwisho.

Makipa wazawa wameonyesha viwango, na Fofana anahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuthibitisha kuwa ule ubora wake wa Sudan haujapotea.

MSIKIE IBENGE

Akizungumzia ushindani huo, Ibenge anasema: “Kila mmoja ana kitu cha kipekee, ila wote kwa pamoja ukiwaangalia wana uwezo unaofanana. Ndiyo maana tunagawa baadhi ya mechi ili wacheze; siyo eneo lao tu, kwa sababu hata nafasi nyingine pia uwanjani zina ushindani mkali.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *