DAR ES SALAAM: Serikali imekamata na kuziondoa sokoni bidhaa bandia 99,100 zenye thamani ya Sh bilioni 4 zilizokuwa zikiuzwa kinyume cha sheria nchi nzima.

Akizungumza leo Aprili 7 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ametaja bidhaa hizo kuwa ni vipodozi, vyakula na vifaa vya umeme vya majumbani, huku ukisubiriwa utaratibu wa kuziteketeza.

Waziri Kapinga amesema juhudi za kuzikamata na kuziondoa bidhaa hizo zimefanywa na taasisi mbalimbali ikiwemo Tume ya Ushindani (FCC) ambayo imepewa mamlaka kisheria ya kudhibiti bidhaa zisizofaa sokoni, kwa lengo la kumlinda mtumiaji wa mwisho, na kuipa serikali mapato.

Akizungumzia operesheni iliyofanyika leo Sinza A Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Kapinga amesema serikali imekamata chupa 4080 za pombe bandia aina ya Konyaji.

“FCC walifanya upekuzi katika nyumba ya makazi ambayo ipo Sinza A ilikuwa inatumika kama eneo haramu la kuzalisha vinywaji na vilevi vyenye nembo ya konyaji,” amesema Kapinga.

Aidha, Waziri Kapinga amesema wafanyabiashara wawili wakiwa na galoni zaidi ya 5,000 za ‘oil chafu’ feki wamekamatwa Dar es Salaam baada ya taarifa za uwepo wa mtandao unaozalisha vilainishi bandia.

Amesema hatua hiyo ni juhudi za FCC katika operesheni yao ya Februari 2026 eneo la Kariakoo ambapo wafanyabiashara hao walikuwa wakitumia chapa ya bandia.

“Kuna wanaochukuwa ile ‘original’ wanajaza kwenye chupa ndogondogo na kuwa ambao ‘oil chafu’ wanachukuwa zile ‘package’ za oil ambazo zimeshatumika wanajaza upya,” ameeleza Kapinga.

Pia Kapinga ameeleza kuwa kuna bidhaa zingine zilizokamatwa kutoka katika kampuni mbalimbali ambazo kesi zake zipo mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *