Manchester, England. Beki wa kati wa Manchester United, Harry Maguire, amesaini mkataba mpya utakaomuweka klabuni hapo kwa muda wa mwaka mmoja na kumaliza sintofahamu iliyokuwa ikimzunguka kuhusu mustakabali wake.

Maguire, mwenye umri wa miaka 33, amekubali kuongeza mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza tena miezi 12 mingine, huku akiripotiwa kupunguza mshahara wake wa paundi 180,000 sawa na Sh612 milioni kwa wiki hadi paundi 100,000 (Sh340 milioni) ili kuendelea kubaki Old Trafford.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, beki huyo wa timu ya taifa ya England amesema ni fahari kubwa kuendelea kuitumikia Man United.

Beki wa Machester United, Harry Maguire akisaini mkataba mpya utakaodumu hadi Juni 2027. Picha na Mtandao

“Kuichezea Manchester United ni heshima ya hali ya juu. Ni jukumu linalonifanya mimi na familia yangu kujivunia kila siku.

”Nina furaha kuongeza safari yangu katika klabu hii kubwa na kuendelea kucheza mbele ya mashabiki wetu wa kipekee ili kuunda kumbukumbu zaidi nzuri pamoja, amesema Maguire.”

Beki wa Manchester United, Harry Maguire wakati alipokuwa na Klabu yake ya zamani Leicester City kabla ya kuhamia United 2019. Picha na Mtandao

Maguire alijiunga na United mwaka 2019 akitokea Leicester City kwa ada ya pauni 80 milioni (Sh272 bilioni) iliyokuwa rekodi ya dunia kwa beki wakati huo akisaini mkataba wa miaka sita.

Baada ya kipindi kigumu, beki huyo ameweza kurejea katika kiwango chake chini ya kocha Michael Carrick, na sasa ni tegemeo muhimu katika safu ya ulinzi ya timu hiyo. Amechukua nafasi kubwa hasa kutokana na majeraha ya mabeki wenzake kama Matthijs de Ligt na Lisandro Martínez.

Mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo, Jason Wilcox, amesema Maguire ni mchezaji wa mfano mwenye uzoefu na uongozi unaohitajika ndani ya Manchester United.

Beki wa Manchester United, Harry Maguire amekubali kupunguza asilimia 50 ya mshahara wake ili kuendelea kubaki Old Trafford hadi Juni 2027. Picha na Mtandao

“Harry anaonyesha moyo wa kupambana na nidhamu ya hali ya juu. Uzoefu wake ni muhimu sana kwa kikosi chetu chenye vijana wengi wenye malengo makubwa,” amesema Wilcox.

Awali kulikuwa na uwezekano wa Maguire kuondoka, hasa baada ya Casemiro kutarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu, hali iliyowafanya United kuwa na hofu ya kupoteza wachezaji wenye uzoefu mkubwa kikosini.

Hata hivyo, Maguire ameamua kubaki licha ya kuvutiwa na ofa kutoka klabu mbalimbali ikiwemo West Ham United, AC Milan pamoja na klabu ya Saudi Arabia ya Al Qadsiah.

Uamuzi huo unaonekana kuwa ushindi kwa mchezaji huyo ambaye ameonyesha uvumilivu mkubwa katika kipindi chake cha kupanda na kushuka ndani ya United, ikiwa ni pamoja na kupokonywa unahodha chini ya kocha wa zamani Erik ten Hag.

Kwa sasa, Manchester United wana uhakika wa kuendelea kuwa na beki huyo mwenye uzoefu huku wakipanga kuimarisha maeneo mengine ya kikosi hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *