
Wadau wa maendeleo nchini Pakistan wamedai huenda nchi hiyo ikaondolewa katika mpango wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya kutokana na kukithiri kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wamesema licha ya Pakistan kuwa mnufaika mkubwa wa mpango huo, matukio ya hivi karibuni yakihusisha kukamatwa kwa waandishi wa habari na wanaharakati yanatia dosari.
Wameeleza hayo katika mkutano wao na waandishi wa habari huku wakiwa na vielelezo vya matukio kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.
‘’Kwa muda sasa Pakistan kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na ukitazama sharti la mpango wa Umoja wa Ulaya ni utekelezaji na usimamizi wa masuala ya haki za binadamu,’’
‘’Chini ya mpango huu Pakistan imeahidi kutekeleza kwa ufanisi mikataba 27 ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mpango wa haki za kiraia na kisiasa, mikataba ya kazi chini ya ILO (Shirika la Kazi Duniani),’’ alisema Imran Riaz, kiongozi wa jopo la wadau hao.
Riaz alisema Umoja wa Ulaya unataka nchi husika izingatie uhuru wa kujieleza, uhuru wa mahakama, kuzuia matukio ya utekaji, adhabu ya kifo na haki za wanawake.
‘’Tatizo ndani ya Pakistan lilianza mwaka 2023 baada ya Bunge kupitisha sheria kandamizi na kushuhudiwa watu wakikamatwa huku mahakama ikipewa mamlaka makubwa,’’ alisema Riaz.
Mwaka 2024/25 shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilieleza kuhusu msako wa raia wanaoikosoa serikali nchini Pakistan na kutoa angalizo kuhusu vitendo hivyo.
Pia, hivi karibuni katika mkutano wa kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, shirika la Amnesty International lilieleza matukio ya utekaji nchini Pakistan na kutaja watu waliokamatwa akiwemo mwanaharakati, Dk Mahrang Baloch.