Kibaha. Wachungaji wametakiwa kuhubiri ukweli wa Neno la Mungu bila kuyumbishwa na maslahi ya kifedha, ili kusaidia kurejesha maadili mema ndani ya jamii.

Akihubiri katika ibada ya umoja wa makanisa ya CCT na TEC iliyofanyika Aprili 6, 2026 katika Kanisa la Roma Kibaha, mchungaji wa Kanisa la Moravian Kibaha, Samuel Ndefula amesema baadhi ya wachungaji wamekuwa wakishindwa kuwaambia waumini wao ukweli kuhusu kuacha dhambi kutokana na hofu ya kupoteza msaada wa kifedha kutoka kwa waumini wenye uwezo.

Amesema hali hiyo inachangiwa na ukweli kuwa wachungaji wengi wana vipato vya chini, hivyo wanapopata waumini wanaowasaidia kifedha hushindwa kuwakemea wanapoishi katika dhambi kwa kuhofia watahama kanisa na wao kupoteza msaada huo.

“Kuna wakati baadhi ya wachungaji wanajikuta wakinyamaza pale wanapotakiwa kusema ukweli kwa sababu ya kuhofia kupoteza waumini wanaowasaidia kifedha, hali ambayo si sahihi mbele za Mungu,” amesema Ndefula.

New Content Item (4)

Ameeleza kuwa mwenendo huo si sahihi kwani jukumu la mchungaji ni kuhubiri ukweli wa Neno la Mungu bila kujali hali yoyote, ili kusaidia waumini kubadilika na kuishi maisha yenye kumpendeza Mungu.

Akizungumzia hali ya dunia, Ndefula amesema matukio ya machafuko yanayoendelea ni ishara kuwa dunia inakaribia kufika mwisho na kuwataka viongozi wa dini kuongeza juhudi katika kuhubiri ukweli ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa waumini.

“Ukweli haupaswi kuuzwa kwa sababu ya njaa au uhitaji, bali uhubiriwe kwa ujasiri ili kuwakomboa watu kutoka katika dhambi na kurejesha maadili katika jamii,” amesema Ndefula.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa CCT na TEC Kibaha, Hery Ruma amesema umoja huo umeendelea kuimarisha mshikamano mzuri kati ya makanisa mbalimbali wilayani humo na kusaidia kuleta maendeleo ya kiroho na kijamii.

“Umoja huu ni nguzo muhimu ya kuwaleta pamoja waumini na makanisa tofauti, na utaendelea kudumishwa ili kujenga jamii yenye mshikamano na maendeleo,” amesema Ruma.

New Content Item (4)

Waumini wa Umoja Wa Makanisa ya CCT na TEC Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye ibada ya pamoja iliyofanyika mjini Kibaha,Picha na Sanjito Msafiri

Naye Mwinjilisti Kiongozi wa Kanisa Anglikana Mt. Gabriel Tumbi Kibaha, Ibrahim Suleimam amesema vijana wanapaswa kuuthamini umoja huo kwa kuwa unawasaidia kuwa karibu na kujenga mshikamano miongoni mwao.

Mmoja wa waumini waliohudhuria ibada hiyo, Betha Mwaluko amesema umoja huo umeleta manufaa makubwa kwa waumini kwa kuwaunganisha na kuwafanya washirikiane katika nyakati za shida na furaha.

Umoja wa makanisa ya CCT na TEC ulianzishwa kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya madhehebu ya Kikristo nchini, hususan kati ya makanisa ya Kiprotestanti na Katoliki, ambapo kwa ngazi ya wilaya ya Kibaha umekuwa ukiandaa ibada za pamoja na shughuli za kijamii zinazolenga kukuza upendo, amani na ushirikiano miongoni mwa waumini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *