Kenya. Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Sefu Shabani ‘Matonya’, leo Alhamisi Aprili 9, 2026 alifikishwa mahakamani katika eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa nchini Kenya akikabiliwa na shtaka la ubakaji.

Kwa mujibu wa Daily Nation, imeripoti kuwa upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa Aprili 7, 2026, katika Jengo la Josy Joka Apartments lililopo Nyali, msanii huyo anadaiwa kumuingilia kimwili mwanamke aliyetajwa katika nyaraka za mahakama kwa herufi J.G kwa kutumia nguvu.

Matonya ambaye anafahamika zaidi kupitia wimbo wake maarufu Vaileti, alishtakiwa kwa kosa hilo chini ya Kifungu cha 3(1)(a) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Makosa ya Kingono.

Mbali na shtaka hilo kuu, msanii huyo pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kufanya kitendo kisichofaa kwa mtu mzima. Mahakama iliambiwa kuwa alimgusa mwanamke huyo sehemu zake za siri bila ridhaa yake.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, mahakama ilimruhusu mshtakiwa kupewa dhamana ya Sh500,000 za Kenya (sawa na Sh10 milioni za Tanzania), kwa sharti la kuwepo mdhamini mmoja raia wa Kenya mwenye dhamana ya kiasi kama hicho.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi lolote la kumruhusu mtuhumiwa kuweka dhamana ya fedha taslimu pekee, ukieleza kuwa ni raia wa kigeni, hivyo kuna hatari ya kutoroka.

Waendesha mashtaka waliomba mahakama iamuru mtuhumiwa kuwasilisha mdhamini wa Kenya, kuweka pasipoti yake mahakamani na mamlaka za uhamiaji kupewa taarifa maalumu ili kumzuia kuondoka nchini bila kibali cha mahakama.

Kwa upande wake, wakili wa msanii huyo aliomba mahakama iweke masharti nafuu ya dhamana, ikiwamo kumpa nafasi ya kuweka fedha taslimu, akieleza kuwa mteja wake yuko tayari kuheshimu masharti yote yatakayowekwa na mahakama.

Mahakama ilisisitiza kuwa mshtakiwa atabaki nje kwa dhamana ya Sh500,000 za Kenya akiwa na mdhamini wa kiasi kama hicho. Aidha, iliamuru upande wa mashtaka kuwasilisha nakala za ushahidi na maelezo ya mashahidi kwa mshtakiwa kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi.

Kama sehemu ya masharti ya dhamana, Matonya alitakiwa kuwasilisha pasipoti yake mahakamani na hataruhusiwa kuondoka katika mamlaka ya mahakama bila ruhusa maalumu.

Vilevile, mahakama ilitoa tahadhari kwa mamlaka za uhamiaji ili kumzuia kuondoka nchini humo bila idhini ya mahakama.

Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 30, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *