Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewakutanisha na kuwapatanisha waimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Upendo Nkone na Martha Mwaipaja baada ya mvutano wao wa muda mrefu uliokuwa ukiendelea kupitia mitandao ya kijamii.
Wawili hao wamekutana leo April 10, 2026 katika Ofisi za RC Chalamila ambapo amesema aliliona suala hilo kupitia mitandao ya kijamii na kuona umuhimu wa kulishughulikia kwa karibu ili kurejesha amani na mshikamano miongoni mwa wasanii hao wa injili.
“Tunafahamu dada zetu Upendo na Martha wote ni watumishi wenye vipawa vikubwa kutoka kwa Mungu, na punde nilipoona sintofahamu yao mitandaoni niliona ni vyema kuzungumza nao mmoja mmoja na kuangalia dhamana kubwa waliyonayo kwa mashabiki wao,” amesema Chalamila.
Aidha kwa upande wa mwambaji mkongwe wa nyimbo za Injili Upendo Nkone alimshukuru Martha kwa kumsamehe kutokana na yale yaliyotokea mitandaoni.
“Tunashukuru Mungu kwa kutusaidia leo tumefika hapa kwa ajili ya kumuona Mkuu wa mkoa na kwaajili ya kutatua changamoto ambayo ilitokea mitandaoni. Tunashukuru kwa uongozi kuwa makini wametusaidia na kutusikiliza.
“Mimi nipende kuwashukuru lakini nimshukuru sana Martha Mwaipaja kwa kunisamehe na mimi nimemsamehe katika yale ambayo yalitokea. Pia tunaomba jamii tuliyowakwaza tusameheni watumishi wa Mungu pamoja na viongozi wote tulipowakwaza na tulipo waaibisha,”amesema
Naye Martha Mwaipaja aliweka wazi kuwa amepokea msahama wa Upendo kwa upande wake yamekwisha. Huku akimuomba Upendo amsamehe kama kuna sehemu alimkwaza.
“Mimi pia namshukuru sana muheshimiwa amekuwa baraka sana amefanikisha kulitatua hili. Pia niseme mama yangu Upendo Nkone wewe ni Baraka wewe ni lango naheshimu sana huduma yako.
“Udhaifu wote tunakuwa nao wanadamu kutokea leo nitajilinda, nitajichunga zaidi. Yamkini kuna mahali nilikuumiza ikakaa moyoni na sijui naomba nisamehe kabisa. Mungu atusamehe kwa sababu ametuamini na ametupa hii kazi ili tuseme na jamii, hivyo basi watu wa Mungu watusamehe pia,”amesema Martha
Mbali na mgogoro huo Martha jana Aprili 9,2026 alitangaza kuacha kuimba kwa muda huku akiweka wazi sababu kuwa hayupo sawa kwa sasa.
“Toka mwaka juzi hadi mwaka jana nimepitia mambo magumu sana, nimepitia hali ambayo ni Mungu tu amenisaidi. Naacha kuimba kwa sasa sijajua ni mwaka gani nitaimba tena lakini kwa sasa kuhusu kuimba naacha kwanza ili nikae sawa.
“Ni hayo tuu nilitaka kuwataarifu mnaopenda huduma yangU naomba mnielewe siko sawa niko vibaya, moyo unaniuma nateseka sana,”amesema Martha