
Israel na Lebanon zinatarajiwa kukutana mjini Washington wiki ijayo wakati mvutano ukiongezeka kutokana na mapigano yakiendelea nchini Lebanon na hofu inayoongezeka kwamba usitishaji mapigano dhaifu kati ya Marekani na Iran unaweza kukwama. Mkutano huo unakuja huku kukiwa na mashambulizi makubwa ya anga, ongezeko la majeruhi, na kutofautiana kuhusu wigo wa makubaliano ya amani na usalama wa kikanda.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Israel na Lebanon zitafanya mazungumzo mjini Washington wiki ijayo, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema siku ya Alhamisi, huku jumuiya ya kimataifa ikizidi kuwa na wasiwasi kwamba kampeni ya mabomu ya Israeli inaweza kuvunja makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo tayari ni dhaifu kati ya Marekani na Iran.
Mashambulizi mabaya zaidi ya anga ya Israel nchini Lebanon tangu Hezbollah kuingia katika vita vya Mashariki ya Kati mwanzoni mwa mwezi Machi yaliwaua mamia ya watu siku ya Jumatano, na kuvunja makubaliano dhaifu kati ya Washington na Tehran chini ya saa 48 baada ya kuanza kutumika.
“Tunathibitisha kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani itafanya mkutano wiki ijayo kujadili mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano na Israel na Lebanon,” afisa wa Marekani alisema.
Tangazo hili linakuja huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwaagiza mawaziri wake kuanza mazungumzo ya moja kwa moja na Lebanon, yanayolenga kupokonya silaha Hezbollah inayoungwa mkono na Iran.
Hata hivyo, afisa wa serikali ya Lebanon ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Beirut ilikuwa ikidai suluhu kabla ya kuingia katika mazungumzo yoyote na Israel.
Israel wala Lebanon hazijathibitisha hadharani kwamba mazungumzo na Marekani yatafanyika wiki ijayo. Mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yamekosolewa vikali na maafisa wa Iran na Pakistan, usiku wa kuamkia majadiliano huko Islamabad yanayotarajiwa kuzingatia hitaji muhimu la Marekani: kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz.
Mkuu wa majeshi ya Israel, Eyal Zamir, alitembelea wanajeshi waliotumwa Lebanon siku ya Alhamisi na kuwaambia kwamba Hezbollah imepata “pigo kubwa” kufuatia mashambulizi ya siku iliyopita.
Katika ishara kwamba vurugu zinaweza kuendelea, jeshi la Israel limetoa amri mpya ya kuwahamisha wakazi wa vitongoji vya kusini mwa Beirut siku ya Alhamisi na kutangaza kwamba litashambulia kambi za Hezbollah nchini Lebanon.