Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Harmonize kwa sasa yupo masikioni mwa wengi kupitia wimbo wake mpya, Wewe (2026), ambao moja kwa moja unagusa uhusiano wake na mchumba wake, Kajala Masanja.
Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, katika video ya wimbo huo iliyoongozwa na Director Ivan, kwa mara nyingine tena amempa nafasi Kajala, ukiwa ni utamaduni wake wa muda mrefu.
Wewe si tu wimbo wa mapenzi, bali ni mwanaume anayechagua kuieleza dunia kuhusu mwenza wake akiufurahia uzuri wake, uwepo wake na amani anayompa katika maisha baada ya kupitia magumu mengi.
Ukiwa umetayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic, Harmonize anautumia wimbo huo kukumbusha kuwa uhusiano wa kweli utaendelea kuwa na thamani kuliko fedha, umaarufu, au vitu vya muda mfupi.
Kajala ndiye ameipamba video hiyo kwa sehemu kubwa ikiwa ni takribani miezi minne tangu wamerudiana, na hata Harmonize kumvisha pete ya uchumba kwa mara ya pili, kama ishara ya ukurasa mpya wa uhusiano wao.
Hii (Wewe) inakuwa video ya pili kwa Harmonize kushirikiana na Kajala, na zote zimetoka miezi michache baada ya wao kurudiana, ingawa utararibu huu wa Konde Boy kuwatumia wapenzi wake katika video za nyimbo zake kila mara umekuwa ukikosolewa na baadhi ya mashabiki.
Kwa mara ya kwanza Kajala anatokea katika video ya Harmonize, ilikuwa ni ya wimbo wake, Nitaubeba (2022), katika video hiyo wamevalia kama bwana na bibi harusi wenye furaha kubwa baada ya kufunga ndoa.
Katika wimbo huu, Harmonize anamwambia mke wake kuwa kabla ya kulala, humuomba Mungu amlinde na kumtunza, kwa sababu yeye ni pacha wake wa maisha.
Anaeleza kuwa atakuwa naye bega kwa bega katika nyakati zote wakati wa shida na tabu, furaha na huzuni, shibe na njaa. Wimbo huu unaakisi upendo wa dhati, uaminifu na mshikamano wa kweli katika ndoa.
Ikumbukwe mnamo Februari 2021, ndipo Kajala na Harmonize walithibitisha kwa umma kuwa wao ni wapenzi baada ya tetesi za muda mrefu huku wakiteka mazungumzo katika mitandao ya kijamii.
Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya Harmonize kusitisha ziara yake kimuziki (In The Club Tour) kwa madai kuwa hali yake ya kiafya sio nzuri. Ziara hiyo ilianzia Mwanza na ilipangwa kupita mikoa mingi nchini.
Kwa hiyo, kusitishwa kwa ziara hiyo kukatoa fursa kwa uhusiano wao kukua mbele ya macho ya umma huku kukiwa na mjadala uliojikita katika tofauti ya umri wao (takribani miaka 10), mjadala ambao kwa sasa hausikiki tena.
Hata hivyo, Kajala si mpenzi wa kwanza wa Harmonize kupata nafasi ya kuonekana katika video mbili za mwanamuziki huyo, kuna Sarah kutokea Italia ambaye ni mkewe wa zamani.
Sarah alionekana katika video za nyimbo mbili za Harmonize ambazo ni My Boo Remix (2019) na Niteke (2019) kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, Afro Bongo (2019) yenye ngoma nne.
Ikumbukwe hadi sasa uhusiano wa Harmonize uliodumu kwa muda mrefu ni wake na Sarah ingawa ndoa yao ilidumu kwa muda mfupi, walioana Septemba 2019 na kuachana Desemba 2020 baada ya msanii huyo kukiri kuisaliti ndoa yao.
Kabla ya Sarah na Kajala, awali Harmonize alianza utamaduni huo kipindi yupo na Jacqueline Wolper aliyetokea katika video ya wimbo wake, Niambie (2017) iliyofanyika Afrika Kusini, ingawa muda mfupi baada ya hapo walitangaza kuachana.
Hadi sasa ni warembo wawili tu ambao Harmonize amewahi kuwa na uhusiano nao lakini hakuwatumia katika video yoyote ya wimbo wake, nao ni Briana kutokea Australia, pamoja na Poshy Queen.
Licha ya kukaa na Poshy Queen kwa zaidi ya mwaka mmoja, hakuweza kufanya hivyo ingawa mashabiki wengi waliamini angefanya video na Poshy kutokana anawakubali warembo wa aina hiyo, mathalani ni Caren Simba ambaye ametokea katika video yake, Single Again (2023).
Na hata katika mistari ya nyimbo zake amekuwa akiwasifia warembo waliojaliwa shepu kama Poshy Queen, mmoja wapo ni Vera Sidika kutokea Kenya ambaye alipata umaarufu baada ya kutokea katika video ya wimbo wa kundi la P Unit, You Guy (2012).
Katika wimbo wake, Show Me (2017) akimshirikisha Rich Mavoko, Harmonize aligusia jinsi anavyovutiwa na Vera Sidika, na hata Kajala ambaye baadaye alikuja kuwa mpenzi wake.
“Wakati unakwenda au unarudi wakata kona, nyuma kama katuni za masudi ulivyonona…. Anita macho kama unaniita, saa sita shepu Vera Sidika,” anaimba Harmonize katika vesi ya kwanza tu ya wimbo huo.
“Tena ni mtu wa Gym, shepu ndio linanipa wazimu,” anaimba Harmonize katika wimbo wake aliomwimbia Kajala ‘Mtaje’ unaopatikana kwenye albamu yake ya pili, High School (2021).
Hivyo hadi kuja kuachana na Poshy Queen bila kufanya naye video yoyote licha ya kuwa pamoja kwa mwaka mmoja, kulishangaza wengi maana si utamaduni wake, utamaduni wake ni kufanya video kali na wapenzi wake kama hii mpya ya sasa akiwa na Kajala Masanja.