Kwa sauti tulivu na uangalizi wa karibu kwa kila mtoto, Salwa anasaidia kujenga hali ya utulivu katika mazingira yaliyotawaliwa na hofu, huzuni na sintofahamu. Darasa lake si mahali pa masomo pekee, bali ni mahali ambapo watoto wanaanza kujihisi kuthaminiwa tena.
Uwepo tu wa Salwa huwafanya watoto wahisi kulindwa.
“Bi. Salwa anapokuwepo, tunajihisi salama, na anaturuhusu kueleza kila tunachohisi ndani yetu,” amesema Layan, mmoja wa wanafunzi wake kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa OCHA, ambayo ni Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura.
Ahmed ameongeza, “Anatuelewa hata tusiposema, na anatupa nafasi ya kuzungumza na kucheza bila hofu.”
Darasa hili la muda ni ubia katika OCHA na shirika la kiraia la War Child ambao kupitia Mfuko wa Kibinadamu wa Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa (oPt HF), wanaendelea kusaidia watoto waliokumbwa na migogoro kwa kuimarisha mazingira salama ya kujifunza na ustawi wa kisaikolojia.
Elimu inayozingatia ustawi wa kihisia
Kupitia mbinu ya kujifunza inayozingatia hisia na ustawi wa kijamii, Salwa huwapa watoto nafasi ya kueleza wanachobeba moyoni.
Hufungua mijadala ya mazungumzo, huwasaidia kuzungumzia hofu zao na huunda nafasi ya kucheza, kutafakari na kuwa na ratiba, hatua ndogo lakini muhimu kwa watoto ambao maisha yao yamevurugwa sana.
Salwa amemarisha ujuzi huu kupitia programu inayotekelezwa na Kituo cha Ubunifu cha Walimu huko Gaza kwa kushirikiana na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la War Child, kwa ufadhili wa Mfuko wa Kibinadamu wa OPT unaosimamiwa na OCHA.
Programu hiyo huwapa walimu zana za vitendo za elimu katika mazingira ya dharura pamoja na mbinu za kujifunza zinazozingatia ustawi wa kihisia, ili waweze kuwasaidia vyema watoto wanaoishi katika hali ya migogoro na kuhama makazi yao.
Kwa War Child na washirika wake, msaada huo umekuwa muhimu sana.
“Mfuko wa Kibinadamu wa OPT ni chanzo muhimu cha msaada kwa kazi yetu huko Gaza kwa sababu unatuwezesha kujibu kwa haraka na kuendana na mahitaji ya watoto na familia,” anasema Mratibu Mkuu wa Programu wa War Child katika eneo hilo. “Uwezo huo wa kubadilika ni muhimu sana katika mazingira kama haya, ambapo mahitaji ni makubwa, hali hubadilika mara kwa mara, na washirika wa ndani wanafanya kila wawezalo kuhakikisha huduma zinaendelea.”
Kwa Salwa, mafunzo hayo hayakuwa tu ya kitaaluma, bali pia inamsaidia kubadilisha elimu ya muda kuwa kitu chenye maana Zaidi na sehemu ambapo watoto wanaweza kurejesha hali ya utulivu na matumaini.
Hadithi ya Salwa ni mfano wa wakati ambapo wanawake wanasaidiwa wakati wa mgogoro, kazi zake zinagusa kila mtu.
Ustahimilivu katikati ya changamoto
Nje ya darasa, maisha yake binafsi yanaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa. Salwa anaishi katika mazingira yale yale wanayoishi watoto wake darasani.
Yeye pia amelazimika kuhama makazi kutokana na vita. Ndiye mtegemezi mkuu wa familia yake inayojumuisha mama yake mgonjwa na mwanawe, Zain, mwenye ugonjwa wa kisukari.
Anaishi katika hema dogo huko Gaza baada ya kupoteza nyumba na kazi yake kutokana na vita. Mbali na kugharamia familia, pia anamtunza mama yake na kufuatilia kwa karibu hali ya afya ya Zain.
Hata hivyo, anaendelea kusonga mbele
“Sikuwa na chaguo ila kuwa imara,” anasema Salwa. “Nguvu yangu ilitokana na wajibu wangu kwa mwanangu na kwa nafsi yangu.”
Kati ya hofu kwa afya ya Zain, juhudi za kuhakikisha anapata matibabu, na jukumu la kumtunza mama yake, huchagua kuwa imara kila siku.
Zain, anayesoma darasa la sita, anaeleza fahari yake kwa mama yake,“Mama yangu ndiye usalama wangu… ndiye aliyenifundisha kuwa imara,” anasema.
Kurejesha utu na matumaini
Kwa Salwa, kurejea kazini kumekuwa zaidi ya kipato. Kumemsaidia kurejesha heshima yake, kumwezesha kugharamia matibabu ya mwanawe na kuleta utulivu fulani baada ya miezi ya misukosuko.
Kisa chake pia ni ukumbusho kwamba wanawake wanapoungwa mkono wakati wa migogoro, athari zake huenda mbali zaidi ya mtu mmoja na zinafikia watoto, familia na jamii nzima inayojitahidi kusimama imara.
Kisa cha Salwa kinaakisi ukweli mpana na unaoonekana kote Gaza, wanawake si tu wavumilivu tu, bali wanabeba familia, wanaunganisha jamii na kuunda mazingira ya malezi na mwendelezo wa maisha katika hali ngumu sana.
Mfuko wa Kibinadamu wa OPT unaosimamiwa na OCHA umeundwa kusaidia washirika wa mstari wa mbele ili waweze kutoa msaada wa haraka mahali penye uhitaji mkubwa zaidi.
Unaweza kusaidia wanawake kama Salwa kuendelea kusaidia jamii zao kwa kuchangia.