
Suala hili la kihistoria na nyeti sana limesitishwa. Uingereza imesitisha kurejesha Visiwa vya Chagos nchini Mauritius kutokana na ukosefu wa usaidizi wa Marekani. Hili ni pigo jingine kwa serikali ya Keir Starmer, katika muktadha wa uhusiano ambao ni dhaifu na Donald Trump.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ikiwa uthibitisho zaidi wa mvutano kati ya rais wa Marekani na waziri mkuu wa Uingereza utahitajika, Visiwa vya Chagos ni moja, anaripoti mwandishi wetu huko London, Sidonie Gaucher.
Ili kuelewa, lazima turudi nyuma, tuangali yaliyopita. Visiwa vya Chagos, katika Bahari ya Hindi, ni koloni la zamani la Uingereza. Katika miaka ya 1960 na 70, Uingereza iliwafukuza wakazi wa eneo hilo ili kuruhusu kuanzishwa kwa kituo cha kijeshi kwenye kisiwa cha Diego Garcia, ambacho sasa kinatumiwa kwa pamoja na London na Washington.
Tangu wakati huo, Mauritius imedai uhuru juu ya visiwa hivi, kwa usaidizi wa vyombo kadhaa vya kimataifa. Mnamo mwaka 2025, makubaliano hatimaye yalisainiwa: London ilikubali kurudisha Visiwa vya Chagos kwa Mauritius, huku ikiendelea na mkataba wa miaka 99 wa kukodisha Diego Garcia ili kudumisha uwepo wa kijeshi wa pamoja wa Marekani na Uingereza.
Donald Trump abadili msimamo
Lakini muktadha wa kisiasa ulibadilika, na Donald Trump alilaani makubaliano hayo kama “ujinga mkubwa” na akakataa kuyaunga mkono. Matokeo yake, Marekani haikutia saini, mradi wa kurejesha visiwa hivyo kwa Mauritius sasa umesitishwa.
“Tunaendelea kuamini kwamba makubaliano haya ndiyo njia bora ya kulinda mustakabali wa muda mrefu wa kambi hiyo (kambi ya kijeshi ya Uingereza na Marekani huko Diego Garcia), lakini tumekuwa tukisema kila mara kwamba tungesonga mbele tu ikiwa ina msaada wa Marekani,” amesema msemaji wa Waziri Mkuu Keir Starmer. “Diego Garcia ni mali muhimu ya kijeshi ya kimkakati kwa Uingereza na Marekani.” Kuhakikisha usalama wake wa muda mrefu wa uendeshaji na itabaki kuwa kipaumbele chetu – hiyo ndiyo sababu hasa ya makubaliano haya,” msemaji wa Downing Street almeongeza.
Kituo hiki kilikuwa na umuhimu mkubwa wa kimkakati kwa Uingereza na Marekani wakati wa Vita Baridi na kilichukua jukumu kubwa katika vita viwili vya Marekani nchini Iraq (1990-1991, 2003-2011) na katika kampeni ya mashambulizi ya Marekani ya 2001 nchini Afghanistan.
Mauritius inaahidi kuchukuwa Visiwa vya Chagos
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius Dhananjay Ramful amejibu baada ya Uingereza kusitisha mpango wake wa kurejesha Visiwa vya Chagos kwa Mauritius. “Tutafanya juhudi zozote kutafuta njia zote za kidiplomasia na kisheria ili kukamilisha mchakato wa kuondoa ukoloni katika sehemu hii ya Bahari ya Hindi,” waziri wa mambo ya nje wa Mauritius alitangaza katika mkutano wa Bahari ya Hindi uliofanyika nchini Mauritius. “Hili ni suala la haki,” aliongeza Dhananjay Ramful.
Waziri wa Sheria wa Mauritius Gavin Glover, kwa upande wake, alisema kwamba tangazo la London “halikuwa la kushangaza,” akihusisha na uhusiano mbaya kati ya Donald Trump na Keir Starmer. “Tunategemea uhusiano wa Uingereza na Marekani … Marekani na Uingereza zitalazimika kufikia makubaliano,” Gavin Glover alilambia gazeti moja nchini Mauritius.