Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amesema nchi haiwezi kuwa na utalii imara pasipokuwa na amani, akiwataka wananchi kuilinda ili kukuza na kuendelea kunufaika kupitia sekta hiyo.

Malecela alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa tamasha la Same Utalii lililofanyika katika viwanja vya stendi wilayani Same mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema kuwa utalii unachangia kwa kiasi kikubwa kuleta fedha za kigeni na kusaidia katika maendeleo ya nchi.

Alisema kuwa, kuna baadhi ya nchi ulimwenguni serikali zake zinaendeshwa kwa fedha za utalii na kuwataka kulichukulia suala hilo kwa umakini mkubwa.

Alifafanua kuwa misingi ya utalii ni ukarimu kwa wageni na kuwataka wananchi wa Wilaya ya Same kuwa mfano katika ukarimu ili kukuza sekta hiyo wilayani humo.

“Hata sehemu kukiwa na njiwa 10,000 wamejaa lakini jiwe likigonga tu wote wanakimbia kwa hiyo na sisi utalii wetu uanze na sisi wenyewe, Watanzania kuwa na amani ni jambo la msingi sana kwani ndio italeta na kuwakaribisha watalii na itatufanya tuendelee kukua kiuchumi,” alisema Malecela.

Alisema kuwa, kinachotuunga pamoja ni amani na kuwasihi Watanzania kuendelea kuitunza na mambo mengine yatafuata.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, alisema lengo la kuanzishwa kwa tamasha hilo ni kuendelea kutangaza utalii wa ndani, kufungua fursa mbalimbali kwa vijana, na kukuza uchumi wa Taifa.

Alisema tamasha hilo linatangaza uwepo wa wanyama  ambao hawapatikani mahali pengine isipokuwa Same, kama vile faru mweusi anayepatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *