Mchezaji wa soka kutoka Ghana, Dominic Frimpong, ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya majambazi wenye silaha kushambulia basi la timu yake ya Berekum Chelsea Ghana jana Jumapili usiku.

Tukio hilo limeibua upya wasiwasi kuhusu usalama wa wachezaji wakati wa safari za ndani.

Berekum Chelsea imeachwa katika mshtuko baada ya winga Dominic Frimpong kuuawa kwa kupigwa risasi wakati wa shambulio la ujambazi wa kutumia silaha kwenye basi la timu, Chama cha Soka cha Ghana kimesema Jumatatu.

Tukio hilo limetokea Jumapili katika barabara ya Goaso–Bibiani wakati timu ikirejea nyumbani baada mchezo wa ya Ligi Kuu ya Ghana dhidi ya Samartex katika mji wa Samreboi kusini mwa Ghana.

Ligi Kuu ya Ghana ndiyo daraja la juu zaidi la soka katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka klabuni iliyoripotiwa na Reuters, watu wenye silaha walizuia barabara na kufyatua risasi kuelekea basi la timu.

“Tukiwa njiani kurudi Berekum kutoka Samreboi, basi la timu yetu lilishambuliwa na kundi la majambazi wenye silaha waliokuwa wamezuia barabara ili kutuzuia kupita.

“Watu waliovaa barakoa na kubeba bunduki na silaha nzito walianza kulipua risasi kwenye basi letu huku dereva akijaribu kurudi nyuma. Wachezaji na wafanyakazi walikimbilia vichakani vilivyokuwa karibu kujikinga,” ilifafanua taarifa ya Berekum Chelsea.

Chama cha Soka cha Ghana baadaye kilithibitisha kuwa Frimpong mwenye umri wa miaka 20 alifariki katika shambulio hilo, kikielezea kifo chake kama pigo kubwa kwa soka nchini humo.

“GFA imepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nzito habari za kusikitisha za kifo cha Dominic Frimpong wa Klabu ya Soka ya Berekum Chelsea,” chama hicho kilisema.

“Tukio hili la kusikitisha si hasara kubwa tu kwa klabu bali pia kwa soka la Ghana kwa ujumla. Dominic alikuwa kipaji chipukizi chenye matumaini makubwa ambaye kujitolea kwake na shauku yake kwa mchezo huo kulionyesha roho ya ligi,” imesema GFA.

Chama hicho kinachosimamia soka kimesema kitaimarisha mipango ya usalama kwa timu zinazofanya safari za mashindano ya ndani kufuatia tukio hilo.

Shambulio hilo limeibua hofu kuhusu usalama wa timu za michezo zinazosafiri kwa barabara nchini Ghana.

Mwaka 2023, klabu nyingine ya Legon Cities, pia iliripoti kushambuliwa kwa basi lake la timu baada ya mechi dhidi ya Samartex, ingawa hakuna majeruhi waliorekodiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *