Él es un defensa central fuerte. Hivyo ndivyo wanavyomuita huko kwao nchini Colombia kwa maana ya “beki wa kati kitasa” na huyu si mwingine ni Yeison Fuentes Mendoza, beki wa kati anayekipiga katika Klabu ya Azam pale kwa matajiri wa Chamazi.
Mendoza ambaye ni raia wa Colombia aliingia hapa nchini msimu wa 2023/2024 akijiunga na Azam akitokea katika Klabu ya Liones ambayo ndio timu yake alioanza nayo maisha tangu alipokuwa mtoto katika akademi ya timu hiyo.
Fuetens ni miongoni mwa mabeki wa kati bora kwa sasa wanaokipiga katika Ligi Kuu, ukiachana na Ibrahim Bacca na Dickson Job wa Yanga pamoja na Rushine De Reuck wa Simba ambao tayari wameshadhihirisha ubora wao, anayefuata ni beki huyu wa Azam ambaye anazidi kuonesha makali yake huko Chamazi.
Beki wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes Mendoza. Picha na Mtandao
Mkolombia huyu ni beki wa kisasa ambaye mara nyingi huwa hatumii nguvu kwani ni mwepesi wa kumsoma mpinzani na kuingia kwenye mechi akiwa anatambua ubora na udhaifu wa wapinzani wake hivyo kumfanya aweze kukabiliana nao kwa urahisi wakati wa mchezo.
Hadi sasa katika eneo la beki wa kati la Azam, Fuentes na Lusajo Mwaikenda wakishirikiana na mabeki wengine wa pembeni kama Pascal Msindo na Mohamed Twalib, wameonesha uimara mkubwa katika kulinda lango la timu yao dhidi ya mashambulizi ya wapinzani waliokuwa wakikutana nayo.
Mpaka sasa Azam imeshacheza idadi ya mechi 17 za Ligi Kuu, lakini timu hiyo imeruhusu idadi ya mabao matano tu ambayo ndio yametikisa nyavu zake ikiwa ni Klabu ya pili kuruhusu mabao machache katika Ligi Kuu wakati namba moja ikiwa ni Yanga ambayo hadi sasa imesharuhusu mabao matatu pekee katika michezo 18 iliocheza.
Beki wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes Mendoza, Picha na Mtandao
Katika michezo 17 ya Ligi Kuu ambayo Azam imecheza hadi sasa, Fuentes ametumika katika michezo 11 ambayo Azam ilishinda mechi sita, ikitoka sare mechi tano bila kupoteza mechi huku ikicheza mechi saba bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa wakati ni mechi ni mechi nne tu ambazo Azam iliruhusu nyavu zake kutikiswa.
Kwa ujumla Azam imeruhusu idadi ya mabao matano katika michezo menne tofauti ya Ligi Kuu ambayo ni dhidi ya JKT Tanzania ilipomaliza kwa sare ya 1-1, sawa na mechi dhidi ya Namungo ambayo nayo ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Mchezo mwingine ulikuwa ni dhidi ya Pamba Jiji ambao wenyewe ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 wakati mechi nyingine ni ile iliocheza na Singida BS ilipomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika dimba la Airtel.
Beki wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes Mendoza. Picha na Mtandao
Mbali na michezo hiyo ya Ligi Kuu, Fuentes pia aliisaidia Azam kukata tiketi ya kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na katika mechi za makundi ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya Klabu Afrika, beki huyu alicheza michezo yote ambapo Azam ilichomoza na ushindi katika mechi tatu na kukubali vipigo vitatu ambavyo ilivipata kutoka kwa AS Maniema na Wydad Athletic Club huku yenyewe ikishinda mechi mbili dhidi ya Nairobi United kwa bao 1-0 nyumbani na ugenini na ushindi mwingine kama huo iliupata dhidi ya AS Maniema kwa kuichapa bao.
Fuentes bado anaendelea kuonesha makali yake huko Chamazi kwani hadi sasa amekuwa ni mmoja ya walinzi wa kati wa kutegemewa sana ndani ya kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na kocha Florent Ibengé ambaye alitua kwenye Klabu hiyo msimu huu akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan ambako alifanya makubwa katika kipindi cha misimu mitatu aliyodumu kwa Waarabu hao.
Beki wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes Mendoza (wa kwanza mbele) akishangilia pamoja na wenzake. Picha na Mtandao
Beki huyu si tu mzuri katika kuzuia mashambulizi lakini pia yuko vizuri katika kuanzisha mashambulizi pale anapokuwa anapoka mpira kwa mpinzani na kutoa pasi hatari kwa viungo na washambuliaji katika maeneo ya pembeni na katikati ya uwanja.
Fuentes alizaliwa Julai 11, 2002 katika mji wa kale na wakihistoria wa Cartagena uliopo Kaskazini mwa Colombia unaosifika kwa umaarufu wake wa kuvutia watalii wengi kutokana na majengo ya kikoloni ya karne ya 16 yenye rangi za kuvutia yaliyojengwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Hispania.