
Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, amesema hana hofu yoyote na Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia mashambulizi ya maneno yaliyotolewa na kiongozi huyo wa Marekani dhidi yake.
Kauli ya Papa Leo XIV inakuja wakati tofauti kati ya viongozi hao wawili zikizidi kuongezeka, hasa kuhusu msimamo wa Vatican dhidi ya vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israel dhidi ya Iran Mashariki ya Kati.
Papa Leo amekuwa akisisitiza umuhimu wa amani na mazungumzo, huku akilaani matamshi ya kisiasa yanayochochea migogoro.
Katika ujumbe mkali kupitia mtandao wa Truth Social, Trump amemshambulia Papa kwa kumuita dhaifu katika suala la uhalifu na mbaya kwa sera za nje. Kauli hiyo imezua mjadala kimataifa, hasa miongoni mwa waumini wa Katoliki na wachambuzi wa siasa.
Hali ilizidi kuwa tete baada ya Trump kuchapisha picha iliyotengenezwa kwa teknolojia ya akili bandia (AI) ikimuonyesha akifanana na Yesu Kristo, hatua iliyokosolewa vikali na makundi ya kidini na hata baadhi ya wafuasi wake.
Aidha, Trump amezua utata zaidi kwa kudai kuwa Papa Leo alichaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa sababu ya uraia wake wa Marekani, akisema: “Kama nisingekuwa Ikulu, Leo asingekuwa Vatican.” Kauli hiyo imeonekana kudharau mchakato wa uchaguzi wa Papa na kuzua hisia kali.
Kauli ya Papa
Akizungumza akiwa safarini kuelekea Algeria katika ziara yake ya siku 11 barani Afrika, Papa Leo amesema hataki kuingia kwenye mabishano ya kisiasa na Trump, bali ataendelea kusimamia ujumbe wa amani.
“Sina hofu na utawala wa Trump, wala kusema kwa sauti ujumbe wa Injili… Nipo hapa kuhubiri amani,” amesema Papa Leo.
Papa huyo amekuwa mkosoaji wa vita dhidi ya Iran, akieleza kuwa vitisho vya Trump vya kuangamiza ustaarabu wa Iran ni visivyokubalika na kumtaka atafute njia ya kupunguza mvutano huo.
Kwa kawaida, ni nadra kwa Papa kujibu moja kwa moja kauli za viongozi wa kisiasa, jambo linalofanya mvutano huu kuwa wa kipekee.
Msisitizo wa Papa
Papa Leo amesisitiza kuwa jukumu lake si la kisiasa bali la kiroho, akilenga kulinda utu wa binadamu na kuhimiza suluhu za amani.
“Watu wengi wanateseka duniani… kuna njia bora ya kushughulikia migogoro kuliko vita,” amesisitiza.
Papa huyo pia amewahi kukosoa sera kali za uhamiaji za Trump, akihoji kama mtu anaweza kujiita mtetezi wa uhai huku akiunga mkono kile alichokiita unyanyasaji wa wahamiaji.
Wakosoaji wamkosoa Trump
Kauli za Trump zimezua mjadala miongoni mwa Wakatoliki duniani. Baadhi ya wachambuzi wamesema mashambulizi hayo hayajawahi kushuhudiwa hata katika nyakati za viongozi wa kimabavu wa karne ya 20 kama Adolf Hitler na Mussolini.
Historia ya uhusiano wao
Hata hivyo, Trump aliwahi kupongeza kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Francis Prevost akisema ni heshima kubwa kwa Marekani kupata papa wa kwanza kutoka nchi hiyo.
Papa Leo, mwenye umri wa miaka 69, alizaliwa Chicago na kufanya kazi ya umishonari nchini Peru kabla ya kuchaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya Wamarekani milioni 70 ni Wakatoliki, sawa na asilimia 20 ya idadi ya watu nchini humo.