Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake wajasiriamali kwa kuwaondolea vikwazo na kurahisisha taratibu za urasimishaji wa biashara ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika maadhimisho ya Women In Balance Kitchen Party Gala 2026, akieleza kufurahishwa kwake kushiriki kwa mara ya kwanza katika jukwaa hilo linalowaunganisha wanawake wajasiriamali kutoka ngazi mbalimbali.

Amebainisha kuwa jukwaa hilo limekuwa na mchango mkubwa kwa zaidi ya miaka 16 kwa kuwaunganisha wanawake wenye mitaji midogo, ya kati na hata wanaojihusisha na biashara za ndani na nje ya nchi, hali inayochochea maendeleo yao kijamii na kiuchumi.

“Jukwaa hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake kijamii na kiuchumi. Limekuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha na kuwawezesha wanawake kuinuana,” amesema Waziri Kapinga.

New Content Item (1)

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judithi Kapinga akikabidhi tuzo kwa mmoja wa wanawake wajasiriamali ili kutambua mchango wake, katika halfa hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanawake, Kapinga amesema bado wapo wanaohofia kurasimisha biashara zao kutokana na mtazamo wa ugumu wa taratibu. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Serikali imebadili mwelekeo na sasa inalenga kuwawezesha wafanyabiashara badala ya kuwaadhibu.

“Zama za kufungia biashara zimekwisha. Tukimkuta mama anafanya biashara bila leseni, tutamwelekeza na kumsaidia kupata vibali vinavyohitajika. Lengo letu ni kuwawezesha, si kuwaadhibu,” amesisitiza.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kusogeza karibu taasisi zinazohusika na biashara, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara, hususan wanawake na vijana.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, akisisitiza kuwa wao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa maono ya Taifa ya kujenga uchumi imara.

Ameongeza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, huku akiwahamasisha wanawake kuwa mstari wa mbele katika biashara na uwekezaji.

“Wanawake ni jeshi kubwa. Tukiamua, tunaweza. Mafanikio ya mwanamke yapo mikononi mwake kupitia ushirikiano na kujituma,” amesema.

Aidha, amepongeza waandaaji wa jukwaa hilo kwa kuendelea kuwa chachu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii, na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika juhudi za kuinua wanawake.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Vida Nasari amesema washiriki 200 walihudhuria tukio hilo na wengi wao ni wanawake wenye ushawishi katika jamii.

Amesema washiriki hao wapo tayari kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani nchini (FCC), ili kupata elimu na taarifa sahihi zitakazowawezesha kusonga mbele.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utakuwa mwanzo wa safari ya kuwajengea wanawake uwezo zaidi kiuchumi na kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *