Kibaha. Mafunzo ya siku tano kuhusu uzalendo, usalama wa nchi, mipango ya sekta za umma, uratibu na mawasiliano yameanza leo Aprili 13, 2026, Kibaha Mkoa wa Pwani yakiwakutanisha washiriki 40 kutoka taasisi mbalimbali za umma zikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika (COASCO).
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Mercellina Chijoriga, amesema mafanikio katika utendaji wa kazi yanahitaji ubunifu, uchapakazi na juhudi za makusudi za kutafuta vyanzo vipya vya mapato.
“Ninyi ni viongozi wa taasisi za umma, epukeni vitendo vinavyoweza kuleta hasara kwenye taasisi zenu. Kuweni wabunifu wa kuanzisha miradi yenye tija kwa serikali, na katika utendaji wenu jitahidini kushirikisha watu mnaowaongoza, msiwe miungu watu,” amesema Profesa Chijoriga.
Amesisitiza pia umuhimu wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma akibainisha kuwa matumizi mabaya ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kuhusu uzalendo kutoka Taasisi za umma wakifuatilia mada mbalimbali. Picha na Sanjito Msafiri
“Itashangaza mkitoka hapa mkirudi kwenye maeneo yenu ya kazi baadae ikasikika kuna changamoto za upotevu wa fedha za umma kwakuwa mtapata mafunzo ni vema ikawe nguzo yenu na mwangaza katika utekwlezaji wa majukumu”amesema.
Baadhi ya washiriki wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bahati Kidai kutoka Shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika (COASCO) amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati sahihi.
“Tunashukuru kwa mafunzo haya, tunaamini yatatuongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu na kuleta mabadiliko chanya katika taasisi zetu,” amesema Kidai.
Kwa upande wake, Cardina Marealle amesema maarifa watakayopata yatasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kuhusu uzalendo kutoka Taasisi za umma wakifuatilia mada mbalimbali. Picha na Sanjito Msafiri
“Mafunzo haya yatatuongezea ufanisi katika utendaji na tutakaporejea tutahakikisha tunaleta mabadiliko yenye tija katika taasisi zetu,” amesema Marealle.
Naye Vicent Bukombe amesema kuwa lengo la kushiriki mafunzo hayo ni kupata uelewa wa pamoja utakaowasaidia kwenda kufanya kazi kwa weledi zaidi kwani wataongezewa mbinu mpya.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo viongozi wa sekta ya umma katika kusimamia rasilimali, kuimarisha mawasiliano na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.