Dar es Salaam. Mabadiliko ya maisha kutoka burudani kwenda kwenye dini yamekuwa yakionekana kwa baadhi ya wasanii na mara nyingi huibua mijadala mikubwa mitandaoni.
Safari hii si ya mtu mmoja pekee, bali imewahi kushuhudiwa kwa watu kadhaa waliokuwa kwenye maisha ya umaarufu, kisha wakaamua kubadili mwelekeo wao.
Miongoni mwao ni Snura, ambaye aliacha muziki na kuamua kujikita zaidi katika dini. Pia kumekuwa na mifano ya wengine kama Gigy Money, ambaye hatua yake ya kusilimu imezua mjadala mkubwa, huku mashabiki na wadau wa burudani wakifuatilia kwa karibu kuona kama ataweza kuendana na mabadiliko hayo.
Mwananchi limekutana na Snura na alishindwa kuficha hisia zake juu ya alichofanya Giggy. Anasema ana furahi kuona mtu mwingine kutoka kwenye tasnia hiyo akichukua uamuzi wa kuingia katika dini, pia alisisitiza umuhimu wa kudumu kwenye maamuzi hayo.
“Nimefurahi sana kuona Gigy ameingia kwenye dini. Hii ni hatua kubwa sana na si jambo rahisi kama watu wanavyofikiria.”
Anaendelea kusema changamoto kubwa si kuingia tu kwenye dini, bali ni kuishi kulingana na mafundisho yake kila siku.
“Kikubwa ninachomwombea ni aweze kushikamana na dini kwa dhati. Wengi wanaingia, lakini changamoto inakuja kwenye utekelezaji, hivyo namwombea sana asiwe ameingia halafu akaacha kufuata yale yanayotakiwa.”
Snura pia anagusia uzoefu wake binafsi, hata yeye mwanzoni hakuwa anaishi maisha ya dini ipasavyo licha ya kuwa tayari ni muumini. Hali hiyo ndiyo inayomfanya awe na hofu kidogo, pia matumaini kwa wale wanaoanza safari hiyo.
“Hata mimi mwanzo nilikuwa muislamu lakini sikuwa naishi kiislamu kama inavyotakiwa. Ndiyo maana namuombea sana Gigy ashike dini kweli kweli.”
Kwa upande mwingine, Snura anaamini mabadiliko ya mtu maarufu yanaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii inayomzunguka, hasa mashabiki wake.
“Ninaamini kabisa hata mashabiki wake wanaweza kubadilika. Wasanii wana nguvu kubwa sana ya kushawishi watu, hivyo akisimama vizuri kwenye dini, wengi watafuata.”
Mbali na Gigy, Snura anaonyesha tamanio lake la kuona wasanii wengine wengi wakibadili mwelekeo wao na kuanza kufanya mambo yenye kumridhisha Mungu.
“Natamani sana na wasanii wenzangu waje tufanye mambo ya Allah. Kikubwa ni dua, Mungu anaweza kuwagusa mioyo yao kama alivyofanya kwa wengine.”
Kwa jumla, Snura anaona mabadiliko haya kama mapambano ya kiroho yanayohitaji msaada wa dua, uvumilivu na msimamo thabiti. Anaamini kila mtu ana nafasi ya kubadilika, lakini mafanikio ya mabadiliko hayo yanategemea jinsi mtu anavyoamua kuyashikilia kwa vitendo.
Katika ulimwengu wa leo na burudani ina mvuto mkubwa, hatua ya wasanii kama Snura na Gigy Money inaendelea kuwa somo kwa wengi kuwa inawezekana kubadilisha mwelekeo wa maisha na kutafuta furaha ya kweli katika imani.
Baadhi ya mashabiki wake katika mitandao ya kijamii wameonyesha kumuunga mkono, huku wengine wakisema wanasubiri kuona kama ataweza kudumu kwenye mabadiliko hayo. Wengine waliandika hatua hiyo ni ya kuigwa, huku wakimtaka azidi kuwa na msimamo katika maisha yake mapya.
Ikumbukwe Snura aliwahi kuwa miongoni mwa wasanii waliotikisa kwenye muziki wa burudani kabla ya kuamua kuachana na maisha hayo na kuchagua njia ya dini, jambo lililowashangaza wengi wakati huo na kuibua mijadala mikubwa miongoni mwa wadau wa burudani.
Wengi wanaamini changamoto kubwa kwa wasanii wanaobadilika ni mazingira wanayotoka, kwani mara nyingi huzungukwa na ushawishi wa kurejea katika maisha ya zamani. Hali hii inahitaji msimamo thabiti na imani ya kweli ili kuweza kushinda vishawishi hivyo.
Hata hivyo, Snura alisisitiza dua ina nafasi kubwa katika safari hiyo, akiamini Mungu ndiye anayebadilisha mioyo ya watu na kuwapa nguvu ya kusimama katika maamuzi yao.
Hatua ya wasanii kama hawa inaendelea kuwa gumzo, na wengi wakisubiri kuona ni nani mwingine atafuata nyayo hizo katika siku zijazo.