Ripoti hiyo kutoka Brazzaville, Kongo na Geneva, Uswisi iliyochapishwa kwenye wavuti wa WHO Afrika inaeleza kuwa watoto zaidi ya milioni 500 walilindwa kupitia chanjo za kawaida kati ya mwaka 2000 na 2024. 

Katika kipindi hicho, nchi 44 za Afrika zilianzisha dozi ya pili ya chanjo ya surua, hatua iliyoongeza kiwango cha chanjo kutoka asilimia 5 mwaka 2000 hadi asilimia 55 mwaka 2024. Kampeni za ziada ziliwezesha utoaji wa dozi milioni 622, na hivyo kupunguza vifo vya surua kwa nusu na visa kushuka kwa asilimia 40.

Mwaka 2025, nchi za Cabo Verde, Mauritius na Seychelles zilifikia hadhi ya kutokomeza kabisa surua na rubela, ikiwa ni hatua muhimu kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa ujumla, chanjo sasa zinakinga dhidi ya magonjwa 13 yanayozuilika kwa chanjo, kutoka magonjwa 8 mwaka 2000. Vifo vya uti wa mgongo vimepungua kwa asilimia 39, huku chanjo ya malaria ikianzishwa katika nchi 25. Mwaka 2024 pekee, chanjo ziliokoa maisha milioni 1.9, ambapo asilimia 42 ilitokana na chanjo ya surua.

Hata hivyo, changamoto zinaendelea, ikiwemo mifumo dhaifu ya afya, ukuaji wa haraka wa idadi ya watu, na athari za mabadiliko ya tabianchi. WHO na Gavi zinasisitiza umuhimu wa uwekezaji zaidi na mifumo imara ya chanjo ili kufikia lengo la asilimia 90 ya chanjo ifikapo 2030 na kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *