Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 15,000 wameuawa tangu mapigano yalipozuka upya Aprili 2023, ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi.

Watu wengine zaidi ya milioni 8.8 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani nchini mwao, huku zaidi ya milioni 3.5 wakikimbilia nchi jirani kama wakimbizi, ikiwemo Chad, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Mwanamke mwenye tabasamu kutoka Sudan akiwa amevaa hijab ya rangi ya zambarau ameketi nje ya nyumba ya udongo, mikono yake ikionyesha ishara wakati akizungumza. Picha hii inahusiana na juhudi za misaada ya kibinadamu nchini Sudan na Chad.

Khadija, mama wa watoto wanane aliyekimbia kutoka El Fasher,sasa anapata hifadhi Tawili Darfur Kaskazini katika makazi ya wakimbizi.

Hivi sasa Mashirika ya misaada yanasema watu milioni 19 wanakabiliwa na njaa kali, huku baadhi ya maeneo yakishuhudia hali ya baa la njaa.

Katika eneo la Darfur na kwingineko, raia wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita wakilazimika kukimbia mara kadhaa bila chochote Kwenda kusaka usalama.

Khadija, mama wa watoto wanane aliyekimbia kutoka El Fasher, sasa anapata hifadhi Tawili Darfur Kaskazini katika makazi ya wakimbizi anaelezea hali ya maisha ya kila siku.

“Tulikuwa El Fasher wakati vita vilipoanza. Hali ilikuwa mbaya sana. Unaweza kupata chakula kwa watoto au wakose kabisa. Hakuna ajira. Msaada pekee tunaopata unatoka kwa shirika la WFP.”

Carl Skau Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP ambaye ametoka Sudan hivi karibuni anasema  jumuiya ya kimataifa  haijafanya vya kutosha kuwanusuru watu wa Sudan kwani imeshindwa kuzuia na kumaliza mgogoro huu na kulinda raia dhidi ya ukatili.

Katika mpaka kati ya Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati, zaidi ya wakimbizi 35,000 kutoka Sudan wamesaka hifadhi, kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA

Fatna Saleh Youssouf, ambaye alipoteza mguu wake vitani nchini Sudan.

Vita vya Sudan vinaingia mwaka wa nne

Miongoni mwao ni Fatna Saleh Youssouf, ambaye alipoteza mguu wake vitani lakini sasa anajaribu kujenga upya maisha yake na mwanaye katika makazi ya wakimbizi ya Birao kwa kujishughulisha na ujasiriamali anasema 

“Nauza maandazi kila asubuhi. Baada ya kuuza… naweza kupata faida ya dola moja au mbili za Marekani. Niliteseka sana nilipofika hapa. Nilipoteza mguu wangu wakati wa vita Sudan. Mlupuko ulipiga nyumba yetu. Lakini niña matumaini ninachotamani ni vita kuisha”

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa hali inazidi kuwa mbaya. Kupanda kwa bei ya mafuta na usumbufu wa njia za usafirishaji kutokana na mvutano wa Mashariki ya Kati kunachelewesha usafirishaji wa chakula na kuongeza gharama  hali inayotishia shughuli za misaada ya kibinadamu.

Kwa mamilioni ya Wasudan, miaka mitatu ya vita haijaleta afueni  bali imeongeza njaa, ukimbizi na hali ya kutokuwa na uhakika na mustakabali wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *