
Mkutano huo unawakutanisha viongozi kutoka Umoja wa Mataifa, akiwemo mkuu wa misaada ya kibinadamu Tom Fletcher, pamoja na wadau kutoka Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya na mataifa makubwa kama Ufaransa, Uingereza na Marekani.
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X Fletcher ameandika hivi “Mkutano wa Sudan unaanza mjini Berlin. Watu milioni 34 wanahitaji msaada wa kibinadamu baada ya miaka mitatu ya vita visivyo na maana. Jaribu la leo ni je, tunaweza kupata maendeleo yanayoweza kupimika kuelekea amani, kukomesha mtiririko wa silaha, na kufadhili msaada wa kibinadamu kwa jamii? Sudan inahitaji hatua, si maneno.”
Mapigano yaliyoanza tarehe 15 Aprili 2023 yameifanya Sudan kuwa katika kile Umoja wa Mataifa unachokitaja kama janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.
Licha ya juhudi za kimataifa, bado kuna upungufu mkubwa wa fedha za misaada. Takribani watu milioni 33 wanahitaji msaada, huku zaidi ya dola bilioni 2.4 zinazohitajika kufanikisha operesheni za kibinadamu zikikosekana.
Kwa mara ya kwanza, mkutano huo unaofanyika Berlin utatoa fursa kwa wananchi wa Sudan wenyewe kutoa ya moyoni lengo likiwa ni kusukuma mbele mpito wa uongozi wa kiraia. Takribani wawakilishi 40 wa kiraia wanatarajiwa kushiriki.
Hata hivyo, bado haijulikani kama mkutano huo utaleta mafanikio makubwa, wakati vita vikiendelea, watu wakikimbia makazi yao, na mateso ya raia yakizidi kuongezeka.
WFP
Carl Skau ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP ambaye alikuwa ziarani nchini Sudan amesema “Naondoka Sudan baada ya wiki moja za kuzuru nchini kote. Jumuiya ya kimataifa imewaangusha watu wa Sudan; imeshindwa kuzuia mzozo, na kuwalinda raia. Kukomesha vita na kutoa msaada wa kuokoa maisha ndio jambo dogo zaidi linaloweza kufanywa.”
WHO
Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni lenyewe linatumia hashtag isemayo Miaka mitatu ni mingi sana. Hoja kubwa ya WHO ni kuwa “vita hivyo vimevuruga huduma za msingi, mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao na kuharibu mfumo wa afya. Sudan inakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani lililojaa magonjwa, njaa, watu kuhama makazi yao na kukata tamaa. Watu wa Sudan wanahitaji amani.”