Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz (36), pamoja na mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Mr. Flavour (43), hadi sasa tunaweza kusema wamepata matokeo mazuri ya kazi zao tatu walizoachia.

Mara nyingi imekuwa ikiaminika kuwa nyimbo nyingi ambazo Diamond anashirikiana na wasanii wengine zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na ushawishi wake katika tasnia ya muziki.

Na ndivyo ilivyo kwa baadhi ya wanamuziki wenzake akiwAmo Flavour, zamani Mr. Flavour ambaye watu wengi hasa Bongo walimfahamu kupitia wimbo wake, Nwa Baby (Ashawo Remix) (2011).

Wimbo huu unaoelezea wanawake wenye tabia ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengi kwa wakati mmoja, Billboard iliuweka nafasi ya tatu kwenye orodha ya nyimbo 50 bora za Afrobeats za muda wote.

Baada ya kuachia albamu yake ya pili, Uplifted (2010), Flavour akawa mmoja wa wasanii wanaotafutwa sana barani Afrika huku akipata nafasi ya kutumbuiza katika matamasha mengi makubwa.

Kipindi unavuma bado Diamond hakuwa si lolote, si chochote katika soko la muziki Afrika, ndio kwanza ilikuwa ni takribani miaka miwili tangu ametoka rasmi kimuziki lakini leo hii stori ni nyingine kabisa tunavyoweza kuzungumza kuhusu wasanii hawa.

Akiwa ameianza safari ya kuupeleka muziki wake kimataifa kufuatia mafanikio ya kolabo yake na Davido, Number One Remix (2013), Diamond aliona msanii mwingine mwenye uzito sawa na Davido ni Flavour.

Basi mipango ikafanyika na mwisho wa siku Diamond akaja kumshirikisha Flavour katika wimbo wake, Nana (2015) ambao ulitayarishwa na Nahreel kutokea The Industry ingawa jina lake halikutajwa katika wimbo huo, kitu kilichoibua minong’ono.

Video yake ilifanyika Cape Town nchini Afrika Kusini chini ya usimamizi wa Director Godfather ambaye ndiye aliyeandaa ile ya Flavour, Nwa Baby (Ashawo Remix) (2011).

Kwa mujibu wa meneja wa Diamond ambaye sasa ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Babu Tale, video ya wimbo ‘Nana’ iligharimu Dola40,000, wastani wa Sh100 milioni kwa sasa.

Hivyo uwekezaji waliofanyika katika wimbo huo si kinyonge hata kidogo, na matokeo yake kwa kazi hiyo na nyingine zilizofuatia kati ya Diamond na Flavour, mambo hayakuwa kinyonge.

Mnamo Agosti 2024, video ya Nana ilifikia rekodi ya kutazamwa (views) mara milioni 100 YouTube ikiwa ni kazi ya tano ya Diamond kufanya hivyo katika mtandao huo.

Kwa matokeo hayo, Diamond akaungana na Burna Boy na Wizkid katika orodha ya wasanii wenye nyimbo tano zilizopata ‘views’ milioni 100 YouTube, huku akiwa ndiye msanii pekee Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo.

Hata hivyo, Nana ulikuwa ni wimbo wa pili kwa Diamond aliyofanya na Flavour kutazamwa mara milioni 100 YouTube baada ya ule uitwao Time to Party (2018) ambao video yake ilifanyika Los Angeles, California nchini Marekani.

Time to Party ni wimbo uliotoka miaka mitatu baada ya Nana, awamu hii ikiwa ni Flavour kamshirikisha Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi.

Na hadi sasa huo ndio wimbo pekee wa Flavour uliofanikiwa kugonga ‘views’ milioni 100 YouTube, hivyo ushirikiano wao kila mara unatoa matokeo makubwa.

Baada ya mafanikio ya Nana (2015), na Time to Party (2018), Diamond na Flavour wakaingia tena studio na kurekodi kolabo yao ya tatu, Berna Reloaded (2021) ambayo Fally Ipupa kutokea DR Congo naye alisikika ndani yake.

Ngoma hii ilifanya vizuri hadi kushinda tuzo ya All Africa Music Awards (AFRIMA) 2021 katika kipengele cha Kundi Bora Kiuchezaji Afrika (Best Artiste, Duo or Group in African Dance or Choreography), na pia uliwania Video Bora Afrika.

Hivyo Diamond na Flavour, mwanzilishi wa 2nite Music Group, wakikutana katika kazi si kinyonge hata kidogo. lima hatua kubwa ipingwa kupitia ushirikiano wao ambao sasa umebeba zaidi sura ya kibiashara.

Mbali na Flavour na Davido, Diamond ameshirikiana na wasanii wengine wa Nigeria kama P-Square, Iyanya, Adekunle Gold, Teni, Tiwa Savage na Rema, mshindi wa MTV VMAs 2023 kupitia kolabo yake na Selena Gomez (Calm Down) ambayo ina ‘views’ bilioni 1.3 YouTube.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *