Mwanza. Wananchi wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wameeleza namna mikopo umiza inavyoathiri maisha yao, familia na uchumi wa kaya, wakati wa kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu mikopo salama na yenye tija inayoendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia kaulimbiu ya ‘Zinduka, Usiuumizwe, Kopa kwa Maendeleo.’
Kampeni hiyo inayolenga kuwaelimisha wakopaji na wakopeshaji kufuata taratibu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taasisi za mikopo zinakuwa na leseni halali ya BOT na zinazingatia kanuni zilizowekwa imetolewa Aprili 17, 2026 wilayani Sengerema.
Akizungumza baada ya kupewa elimu hiyo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mjini Kati, Asha Mlewa, amesema mikopo umiza imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya kifamilia, hasa pale mikopo inapochukuliwa kwa siri bila kuwashirikisha wenza.
Ofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Shaban Shaban akitoa elimu kwa wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu mikopo salama eneo la stendi ya zamani ya Sengerema kupitia kampeni ya Zinduka Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo. Picha na Saada Amir
“Kwakweli mikopo umiza inaumiza sana. Malalamiko ni mengi, watu wanafirisiwa na wakati mwingine mume hajui kabisa. Hali hii inaleta changamoto kubwa katika familia,” amesema Mlewa.
Ameongeza kuwa juhudi zinaendelea kuwafikia wanaume ili waweze kuelewa hali hiyo, kwani wengine huamua kusamehe wenza wao, huku wengine wakichukua uamuzi wa kuachana kabisa.
Kwa upande wake, mkazi wa Sengerema, Restuta Mwandambo amesema ukosefu wa malengo sahihi ya mikopo ni tatizo kubwa linalochangia mateso kwa wakopaji wengi.
“Wanawake wengi wamepoteza makazi yao kutokana na mikopo umiza. Inawezekana ni kwa sababu hatuna malengo sahihi. Tumefundishwa leo kwamba mkopo unatakiwa uwe wa maendeleo, lakini wengine wanakopa kwa matumizi ya kawaida yasiyo na tija,” amesema.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kukopa kwa ajili ya shughuli zinazozalisha kipato ili kuwezesha urejeshaji wa mkopo bila shida.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Sengerema wakisikiliza elimu ya mikopo salama iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania eneo la stendi ya zamani ya Sengerema kupitia kampeni ya Zinduka Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo. Picha na Saada Amir
Mkazi mwingine, Kennedy Deus ameeleza changamoto ya mikataba ya mikopo isiyoeleweka, akisema mara nyingi wakopaji hujikuta wakikubaliana na masharti wasiyoyafahamu kikamilifu.
“Unaweza kusoma mkataba ukaona uko sawa, lakini ukija kwenye urejeshaji unakutana na vigezo vipya ambavyo hukuviona awali. Hii inaleta matatizo makubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa hali hiyo inachangia baadhi ya watu kushindwa kurejesha mikopo na kuamua kukimbia familia zao kutokana na presha ya madeni na riba kubwa.
Kennedy ameiomba BOT kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha wakopeshaji wanazingatia uwezo wa mkopaji pamoja na kuweka viwango vya riba vinavyokubalika.
Awali akitoa elimu hiyo, Ofisa wa BOT, Shaban Shaban amesema taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia taasisi zote za kifedha ili kuhakikisha zinazingatia sheria na kulinda haki za wananchi.
Ameeleza kuwa mwananchi yeyote mwenye malalamiko anapaswa kwanza kuwasiliana na taasisi aliyokopa, kwa kuandika barua ya malalamiko na kuhifadhi nakala yenye saini, endapo hatapata majibu ndani ya siku 14 au hataridhika, anaweza kuwasilisha malalamiko yake BOT kwa hatua zaidi.
“Ni muhimu kufuata utaratibu huu badala ya kukimbilia polisi au mahakamani moja kwa moja, kwani unaweza kupoteza baadhi ya haki zako nyingine,” amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati wilayani Sengerema, Asha Mlewa akizungumzia athari za mikopo umiza kwa wananchi wa kitongoji chake wakati wa elimu ya mikopo salama iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wilayani humo. Picha na Saada Amir
Aidha, ameelekeza matumizi ya mfumo wa mtandao kupitia dirisha la ‘SEMA na BOT’ ambapo mwananchi anaweza kujisajili kwa kutumia taarifa zake binafsi na kuwasilisha malalamiko bila gharama yoyote.
“Msikubali kunyanyaswa na hizi taasisi za kifedha endapo mtapata huduma za mikopo lakini na wewe pia unapokwenda kupata fedha za mkopo hakikisha unazipeleka katika shughuli za kiuchumi usiende kununua nguo,”amesema.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha mikopo wanayoichukua inaelekezwa kwenye shughuli za kiuchumi kama biashara, kilimo au huduma ndogondogo badala ya matumizi yasiyo ya lazima.
Ofisa huyo amewaasa wananchi kuzingatia mambo muhimu kabla ya kuchukua mkopo, ikiwemo kutambua na kuelewa riba halisi na tozo zote za mkopo, pamoja na kupata nakala ya mkataba wa mkopo uliosainiwa na pande zote mbili.
Pia amewataka kuhakikisha wanafanya marejesho kwa wakati ili kuepuka adhabu na gharama za ziada, pamoja na kuepuka kuchukua mikopo kupitia link au ujumbe wa mitandaoni usio rasmi.
Shaban ameeleza kuwa ni muhimu kuhakikisha mkopeshaji wa kidijiti ameidhinishwa na kuorodheshwa kwenye tovuti ya BOT, na kwamba wananchi wanapaswa kukopa kwa malengo ya kimaendeleo ili kuboresha hali zao za maisha badala ya kujiingiza kwenye madeni yasiyo na tija.