
Mwanza. Zaidi ya kaya 20,000 kwenye visiwa kumi vilivyopo jijini Mwanza vinatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme wa nishati ya jua kuanzia mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
Hii ni kufuatia kuelekea kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa jua usiotegemea gridi ya taifa (off-grid), unaolenga jamii ambazo kwa muda mrefu zimekuwa nje ya huduma hiyo muhimu.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Aprili 19, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Rex Energy, Francis Kibhisa, alipokuwa akielezea mradi huo ambao utanufaisha pia biashara zaidi ya 400.
Kibhisa amesema utekelezwaji wa mradi huo ni kufuatia ushindi wa kampuni hiyo katika shindano la ‘Lighting Rural Tanzania’, mpango unaohamasisha matumizi ya nishati ya jua nje ya gridi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Tumeendelea kufanya kazi kwa kasi kubwa katika mazingira magumu ya kijiografia ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya kupanua upatikanaji wa nishati safi na nafuu,” alisema.
“Kwa sasa tuko hatua za mwisho, na ni faraja kubwa kuona jamii za visiwa hivi hatimaye zitaanza kufurahia umeme wa uhakika kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nchi. Hili linahusu kurejesha heshima ya maisha, kuboresha kipato na kufungua fursa halisi za maendeleo,”amesema Kibhisa
Mkurugenzihuyo ameeleza kuwa mradi huo, uliopatikana kupitia mpango wa ushindani wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaolenga kuharakisha upatikanaji wa umeme vijijini kupitia nishati jadidifu na umetekelezwa kwa awamu ili kuhakikisha uthabiti wa mifumo na ubora wa huduma.
Hata hivyo Kibhisa mebainisha kuwa wananchi na wafanyabiashara katika visiwa vya Gana, Kamasi, Bwiro na Bulubi wanatarajiwa kuanza kupata umeme ifikapo mwisho wa Mei mwaka huu, huku visiwa vya Kweru Kuu, Kweru Mto, Izinga, Zeru, Bushengere na Sizu vikitarajiwa kuunganishwa ifikapo Desemba 2026, baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za usimikaji.
“Tulichagua kwa makusudi utekelezaji wa awamu ili kuhakikisha kila kisiwa kinapata mfumo kamili na unaojitegemea kuanzia uzalishaji hadi usambazaji, kila kipengele kimeundwa kukidhi mahitaji maalum ya jamii hizi huku kikihakikisha uendelevu wa muda mrefu.amesema Mkurugenzi huyo”
Kwa mujibu wa Kibhisa miongo kadhaa, visiwa hivyo vimekuwa vikitegemea jenereta za dizeli na mafuta ya taa, hali iliyoongeza gharama za maisha, kudhoofisha shughuli zakiuchumi, pamoja na kuathiri utoaji wa huduma katika shule na vituo vya afya,na hivyo kuchochea umaskini.
Hivyo amesema upatikana kwa umeme huu mpya kunatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya maisha kwa kuongeza muda wa shughuli za biashara, kuwezesha uhifadhi wa samaki kwa kutumia majokofu na hivyo kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuboresha ubora wa mazao, pamoja na kurahisisha matumizi ya nishati safi majumbani. Shule zitaongeza muda wa kujifunza, huku vituo vya afya vikiboresha uhifadhi wa chanjo na uendeshaji wa vifaa muhimu vya tiba.
Aidha Upatikanaji wa umeme katika visiwa hivi ambavyo ni mhimili wa uchumi wa uvuvi wa Kanda ya Ziwa—unatarajiwa kuongeza thamani ya mazao, kuboresha uhifadhi na uchakataji, kupanua masoko na kuvutia uwekezaji mpya uliokuwa ukikwamishwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.
Aidha, amesema mpango huo unaendana na sera za taifa za nishati safi na usambazaji umeme vijijini, zinazolenga kupanua upatikanaji wa nishati endelevu huku ukipunguza utegemezi wa mkaa na dizeli.
Mradi huo unahusisha uwekaji wa mitambo ya sola, mifumo ya kuhifadhi nishati kwa betri, mitandao ya usambazaji, kazi za ujenzi, nguzo za umeme, mita za kisasa, pamoja na kuzingatia viwango vya mazingira chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Kuhusu Rex Energy, Kabhisa amesema ni kampuni ya uhandisi, ununuzi na ujenzi (EPC) pamoja na utoaji wa suluhisho kamili za nishati ya jua yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ikihudumia serikali, taasisi binafsi, mashirika ya kimataifa, pamoja na wateja wa makazi, biashara na viwanda.
Vilevile imechangia maendeleo ya jamii kwa kuboresha huduma za maji, usafi na mazingira (WASH) katika Shule ya Msingi Kamasi, ikiwa ni mwanzo wa juhudi pana za uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika visiwa hivyo.