Dar es Salaam. Kocha wa makipa, Ally Mustapha ‘Barthez’, amejiunga na Singida Black Stars baada ya kukaa nje tangu Desemba mwaka jana, alipoachana na TMA Stars ya Arusha.

Barthez, aliachana na TMA FC, Desemba 25, 2025, baada ya kusitishiwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote mbili kikosini, sambamba na Kocha Mkuu, Habibu Kondo, Kocha Msaidizi, Augustino Thomas na Kocha wa Viungo, Kigi Makasi.

Baada ya kukaa nje kwa takribani miezi minne, uongozi wa Singida umefikia makubaliano ya kumwajiri Barthez, kutokana na uzoefu wake wa kuwafundisha makipa.

Barthez aliyewahi kuzichezea Yanga, Simba, Singida United, Ndanda na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa nyakati tofauti, amejiunga na Singida Black Stars, ili kuongeza ufanisi zaidi kwa makipa, Metacha Mnata na Amas Obasogie.

Kujiunga kwake na kikosi hicho anaenda pia kunaenda kuliongezea nguvu benchi la ufundi linaloundwa na Kocha Mkuu, Muhibu Kanu, Meneja Mkuu, Papy Kimoto na msaidizi wake, Kapiten Ngoyi Dora.

Aprili 5, 2026, Klabu ya Singida Black Stars, ilitangaza kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mkenya David Ouma, kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika mashindano mbalimbali, hususani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026.

Uamuzi huo wa Singida wa kuvunja benchi hilo la ufundi ulifikiwa muda mfupi tu tangu timu hiyo ichapwe mabao 2-0, dhidi ya TRA United, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *