Dar es Salaam. Mrembo kutoka Dar es Salaam, Latricia Ian (24) ametangazwa kuwa Miss World Tanzania wa kwanza baada ya kuwashinda washiriki wengine 19 katika shindano la kihistoria lililofanyika kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Aprili 19,2026.

Kutokana na ushindi huo, Latricia ameondoka zawadi mbalimbali ikiwemo gari aina ya Mercedes-Benz A-Class lenye thamani ya zaidi ya Sh40 milioni, kitita cha fedha taslimu Sh10 milioni, bima ya safari pamoja na taji la ushindi, huku jumla ya thamani ya zawadi zote ikifikia zaidi ya Sh100 milioni.

Zawadi hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Paul Makonda.

Latricia alivalishwa taji hilo kichwani na Miss World anayetawala kwa sasa, Opal Suchata Chuangsri kutoka Thailand, akishirikiana na Miss World Africa, Hasset Dereje Admassu kutoka Ethiopia.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Nouru Masoud, naye kutoka Dar es Salaam, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Paulina Allute kutoka Kanda ya Kati.

Washiriki wengine waliopenya kwenye tano bora ni Silya Mussa kutoka Nyanda za Juu Kusini aliyeshika nafasi ya nne, pamoja na Diana Rutagalinda aliyemaliza katika nafasi ya tano.

Baada ya ushindi huo, Latricia anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World yatakayofanyika nchini Vietnam kuanzia Agosti 9 hadi Septemba 5, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 75 ya mashindano hayo.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *