Video iliyoandaliwa na UNICEF Tanzania inaanza kwa kumwonesha Magdalena A. Prosper, mwenye umri wa miaka 12, akiwa amevaa sare na begi akitoka shuleni. Kisha amekaa nyumbani anakumbuka hali ngumu aliyokumbana nayo kabla ya kupata msaada wa lishe:

“Nilivyokuwa darasani nakuwa yaani mwalimu alipokuwa anafundisha nilikuwa sijisikii vizuri kwa sababu nilikuwa na njaa.”

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watoto kuacha shule kwa muda mrefu, kama anavyoeleza muhudumu wa jamii, Joshua Raineli:

“Wao asubuhi wanaamka wanaona naenda shule lakini matokeo yake wanaona barua ya utoro ya mtoto nawafuata nyumbani… alikuwa ameacha shule takribani miaka miwili au mitatu.”

Kupitia elimu ya malezi chanya, wazazi pia wameanza kubadilika. Mama yake Magdalena, Sophia M. Miselya, anaeleza:

“Mwenzangu nikawa nimekuja kuelimishwa na kikundi cha malezi chanya, nikaamua nimtolee mchango aanze kula shuleni.”

Msichana mdogo wa Kiafrika aliyevaa kanzu nyekundu ameketi nje ya jengo la matofali akiandika katika daftari, huku mwanamke katika picha ya nyuma akichukua maji kutoka kwenye ndoo ya kijani. Picha inayohusishwa na mipango ya chakula cha shule na elimu ya UNICEF nchini Tanzania.

Magdalena A. Prosper, Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 12 kutoka Tanzania.

Baada ya kurejea shuleni, Magdalena anasema hali yake imebadilika kabisa:

“Niliporudi shule nilijisikia vizuri, ninapokuwa nakula chakula napata nguvu za kushirikiana na wengine katika majaribio ambayo tunakuwa tumepewa na mwalimu.”

Walimu na jamii wanasema mabadiliko hayo yanaonekana wazi, huku baadhi ya watoto wakipewa majukumu ya uongozi shuleni ili kuwajenga zaidi.

‘’Kwa hiyo mtoto huyo niliendelea kumfuatilia hadi pa mwalimu mkuu mpaka mwalimu mkuu akawa ananiambia kweli mtake wanaendelea vizuri na wamempa hadi uongozi wa shuleni ili kumsogeza mtoto kupenda nini? kupenda shule.’’

Kwa upande mwingine, elimu ya malezi imewasaidia pia wazazi kubadilisha namna ya kuwalea watoto wao, kama anavyoeleza Restuther Richard.

‘’Mimi binafsi nilikuwa sijui kuzungumza na watoto lakini baada ya kupata haya mafundisho nilijenga kwanza mimi binafsi kabla sijaenda kwenye jamii nikaanza kuzungumza na watoto wangu leo hii watoto wangu tunaishi vizuri tunaheshimiana ndipo nikaanza safari ya kwenda kwenye jamii kutoa elimu.’’

Mama wa Magdalena ana matumaini makubwa kwa mtoto wake:

“Ndoto zangu kwa mwanangu ni kwamba asome afike mbali.”

Naye Magdalena ana ndoto ya kusaidia wengine siku zijazo

“Nikimaliza shule napenda kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto shule ili kupata elimu.”

Simulizi hii inaonesha wazi kuwa lishe bora na malezi sahihi vinaweza kubadili maisha ya mtoto—na hata jamii nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *