
Akizungumza leo katika Jukwaa la Ufadhili kwa Maendeleo linalofanyika chini ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii ECOSOC, Guterres amesema hali hiyo inaongeza mzigo kwa uchumi ambao tayari uko katika hali tete.
“Vita Mashariki ya Kati vinasababisha mshtuko mpya mkubwa kwa uchumi wa dunia,” amewaambia wajumbe, akionya kuwa athari zake “zinaenea kwa kasi katika maeneo na sekta mbalimbali.”
Bei zapanda na mifumo ya kimataifa yatikisika
Guterres ameeleza kuwa mzozo huo unasababisha kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama mafuta, mbolea na chakula, huku pia ukivuruga sekta muhimu kama biashara, usafiri na utalii.
“Tunaona athari za kiuchumi zikienea katika minyororo ya usambazaji kuanzia nishati hadi kilimo na kuathiri mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea,” amesema Guterres.
Ameonya kuwa hali hii inaweza kufuta mafanikio madogo yaliyopatikana katika juhudi za kufufua uchumi wa dunia.
Shinikizo la madeni lawaelemea nchi zinazoendelea
Kwa mujibu wa Guterres, serikali nyingi hasa katika nchi zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto kubwa za kifedha kutokana na kupanda kwa gharama za nishati, ukuaji hafifu wa uchumi na kushuka kwa thamani ya sarafu.
“Fedha za umma zinabanwa kutoka pande zote gharama zinaongezeka, mapato yanapungua, na hatari ya madeni inaongezeka,” ameonya.
Amebainisha kuwa nchi nyingi hazina nafasi ya kifedha ya kukabiliana na mishtuko mipya ya kiuchumi.
Uwekezaji katika vita badala ya maendeleo
Guterres pia amekosoa mwelekeo wa kimataifa wa matumizi ya fedha, akionesha kupungua kwa misaada ya maendeleo huku matumizi ya kijeshi yakiongezeka.
“Tunashuhudia mwenendo wa kutia wasiwasi nchi zinawekeza zaidi katika vita kuliko maendeleo,” amesema.
Ameongeza kuwa “Hali hii si tu ya muda mfupi, bali ni hatari kwa uthabiti wa dunia.”
Pengo la dola trilioni 4 kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu
Katibu Mkuu amesisitiza kuhusu changamoto katika mfumo wa kifedha wa kimataifa, akionya kuwa pengo la ufadhili wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, sasa limezidi dola trilioni 4 kwa mwaka.
“Pengo la ufadhili kwa maendeleo endelevu linaongezeka kwa kasi ya kutisha,” amesema.
Pia amesisitiza kuwa “Bila mageuzi ya haraka na ushirikiano wa kimataifa, SDGs zitabaki ndoto.”
Wito wa hatua za haraka za kimataifa
Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuleta utulivu wa uchumi wa dunia, kusaidia nchi zilizo hatarini, na kurekebisha mifumo ya kifedha ili kuunga mkono maendeleo endelevu.
“Huu ni wakati wa mshikamano na uwekezaji wenye busara si mgawanyiko na mawazo ya muda mfupi,” amesema.
“Lazima tuchague njia inayotanguliza amani, uthabiti na ustawi wa pamoja.”
Mtazamo dhaifu wa uchumi wa dunia
Kadiri mvutano wa kisiasa unavyozidi kuongezeka na shinikizo la kiuchumi kushika kasi, Umoja wa Mataifa unaonya kuwa dunia ipo katika kipindi muhimu kitakachoamua mustakabali wake.
Guterres amehitimisha kwa kusema kwamba “Changamoto hizi zimeunganishwa na suluhu zake lazima ziwe za pamoja”.