
Maelfu ya wanajeshi wa Marekani na Ufilipino, walijiunga kwa mara ya kwanza na kikosi kikubwa zaidi cha wanajeshi wa Japani, kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka, mazoezi yanayofanyika wakati huu vita ya Mashariki ya kati ikitatiza uchumi za dunia.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mazoezi haya yatajumuisha ufyatuaji wa risasi za moto kaskazini mwa Ufilipino kuelekea eneo la bahari ya Taiwan pamoja na eneo la bahari ya kusini ambalo limekuwa kiini cha mvutano kati ya China na Ufilipino, ambapo mara kadhaa meli zao zilikabiliana.
Katika zoezi mojawapo, ambapo Japani inachangia karibu wanajeshi 1400, itatumia makombora aina ya 88 yaliyotumika wakati wa vita ya pili ya dunia.
Zaidi ya wanajeshi 17000 wanashiriki mazoezi haya ya siku 19 yaliyopewa jina Balikatan au ‘bega kwa bega’, na yanahusisha idadi ya wanajeshi sawa na wale waliohusika mwaka jana kutoka nchi za Australia, New Zealand, Ufaransa na Canada.
Wakati mazoezi haya yakianza, China imezionya nchi hizo dhidi ya kile imesema zisijaribu kucheza na moto, ishara kuwa mazoezi haya yanachukuliwa na Beijing kama kitisho kwa usalama wake kutokana na mgogoro wake na Taiwan ambayo inadai ni sehemu yake, na bahari ya kusini ambayo inasema ni sehemu yake.
Marekani imekuwa mstari mbele kusimama na Taiwan pamoja na Ufilipino, ikisisitiza kuwa haitafunga mikono yake litakapokuja suala la kuziunga mkono nchi hizo dhidi ya vitisho vya Beijing.